Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Mradi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhusu ujenzi wa jengo la Ofisi la Makamu wa Rais unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, leo Mei 08, 2023.
Wajumbe wa Menejimenti wakiwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi Makamu wa Rais unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, leo Mei 08, 2023.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama akisaini kitabu cha wageni alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi la Makamu wa Rais unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, leo Mei 08, 2023.(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS).
…..
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Mei 08, 2023.
Akiwa amembatana na Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Mkama ameonesha kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa jengo hilo linalojengwa na Kampuni ya SUMA JKT ikisimamiwa na Mshauri Elekezi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Kaimu Katibu Mkuu amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha watekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati kama ambayo mkataba unavyoonesha.
“Tunawategemea sana katika kukamilisha jengo hili, tunawaomba msituangushe kwani mnapofanya vizuri mnajenga taswira nzuri ya taasisi yenu na Serikali kwa ujumla,” amesisitiza.
Kwa upande wake Meneja Mradi kutoka NHC Mhandisi Robert Kintu ameishukuru Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kufanya ziara ya kutembelea mradi huo kwa lengo la kuangalia maendeleo ya ujenzi huo.
Pia, Mhandisi Kintu amesema kwa niaba ya shirika hilo ambao ndio msimamizi wa mradi huo watayafanyia kazi maelekezo yalitolewa na Kaimu Katibu Mkuu Dkt. Mkama ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakidhidhi viwango kwa mujibu wa mkataba na kukamilika kwa wakati.Ofisi ya Makamu wa Rais ilisaini mkataba wa sh. bilioni 18.8 na SUMA JKT na kuanza ujenzi wa jengo hilo Oktoba 13, 2021 ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2023.
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa jengo hilo kutawezesha watumishi wa Ofisi hiyo kuongeza tija, morali na ufanisi katika usimamizi na utekelezaji wa majukumu yao.