TAASISI ya Islamic Foundation imechimba ambayo imefanikisha mradi wa maji kwa kuchimba kisima kwenye Kata ya Matui Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, imechimba kisima kingine cha maji katika shule ya sekondari Kiteto, chenye urefu wa mita 150 na thamani ya shilingi milioni 45.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, baada ya kuzindua mradi huo, Mkurugenzi wa taasisi ya Islamic Foundation, Ibrahim Twaha, alisema katika mkoa wa Manyara wametekeleza mradi wa visima vipatavyo saba vyenye thamani ya shilingi milioni 270.
Twaha alisema kati ya visima hivyo, visima vinne vimetekelezwa ndani ya wilaya ya Kiteto, kisima kimoja katika kata ya Matui na visima viwili kijiji cha Sukuro wilayani Simanjiro.
“Hili ni jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu pia ni jambo la kumshukuru kiongozi wetu, Rais wetu Dokta John Pombe Magufuli kwa juhudi zake kubwa na ndiyo maana leo mnaona tupo tunatekeleza miradi katika hali ya amani na furaha, hizi zote ni juhudi za kiongozi wetu jemedali wetu Rais John Magufuli, kwa hiyo hili ni jambo ambalo la kumpongeza sana,” alisema Mkurugenzi Twaha.
Alisema lslamic Foundation ni taasisi ambayo iko kisheria nchini imeanzishwa 1998 na hadi sasa wameweza kutekeleza miradi ya visima zaidi ya 3,000 ikiwa ni visima virefu na vifupi.
“Tumeweza kuwanusuru akina mama mbalimbali ambao walikua wanaliwa na mamba katika sehemu za kando kando ya mito, na huduma hizi katika taasisi yetu sisi tunazitoa ni huduma za raia au wananchi watanzania, nje ya kuangalia dini wala kabila, wala chama wala nani, maadamu ni Mtanzania ana haki ya kupata mradi huu, kwenye dini yetu sisi ya kiislam huwa maji ni uhai, mnyama anahitajika apate na watu wote, kwahiyo watanzania wanayo haki kupitia kiongozi wao jemedali Rais Magufuli na kupitia taasisi zote ziwe za kidini, zisiwe za kidini madamu zipo ndani ya Tanzania wanayo haki ya kupata huduma hii, kwa ajili hii napenda nikushukuru sana mheshimiwa mkuu wa mkoa nimefurahi sana leo kuungana na wewe katika zoezi hili nakushukuru sana,” alisema Twaha.
Mbunge wa jimbo la Kiteto, Emmanuel Papian aliishukuru taasisi hiyo Kwanzaa kufanikisha hilo kwani walishapima kuchimba visima 19 kwenye maeneo mengi bila mafanikio ya kupata maji.
“Sisi tunaiwashukuru hii taasisi na tunadhani kwa gharama za mradi huu kwa shilingi mil.45 wanapata maji leo zaidi ya lita 3,000 kwa dakika 45, ina maana sisi tunaweza kufanya hesabu wenyewe ndani ya fedha za wizara za halmashauri zinazoingia (RUASA) ukiwapa hawa kazi wanaweza kutuchimbia maji wakatupa kutujengea visima tukapunguza migogoro ya maji na ubadhilifu wa fedha zinazotokana na wakandarasi tukawa tumepunguza migogoro tukabaki salama, tushirikiane nao hawa watuchimbie, watujengee tuwalipe waondoke tupate maji,” alisema Papian.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti aliipongeza taasisi hiyo kwa kile alichodai jambo hilo sio dogo ni kubwa kwani siyo mara yao ya kwanza kufanya shughuli kama hiyo.
“Nakumbuka nikiwa mkuu wa wilaya Arumeru mlituchimbia visima vingi sana, taasisi hii imekuwa ikitoa msaada mkubwa na tunawashukuru na tunazidi kuwaombea muendelee kufanya hii huduma, kwa sababu hii najua ni ibada kwenu, kwani watoto hawa walikuwa wanateseka sana kutafuta maji, na niwaombe haya maji msiyachezee ovyo ovyo na wala msiyatoe nje ya shuleni hapa kwa sababu Lita 3,000 kwa mahesabu yangu ya haraka haraka bado yanawatosheleza watoto walio hapa, mtoto mmoja kwa siku anatumia lita 60, Lita 20 asubuhi, jioni lita 20 na hapa katikati.
Hata hivyo, alisema taasisi hiyo imekuwa ikihudumia nchi nzima hivyo, hivyo aliwaomba waendelee kuongeza visima vingine ndani ya mkoa huo ili kuweza kupunguza adha ya upatikanaji wa maji, ili kuwapunguzia kusaidia jamii hasa wanawake.