Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akimkabidhi tuzo maalum ya jumla ya Mwanasheria mwanamke kinara Balozi Mwanaidi Maajal ambaye ni Mwanachama wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania TAWLA kwamchango wake katika kusaidia wanawake na watoto kwa msaada wa kisheria na mchangowake katika kuhakikisha TAWLA inafikia malengo yake, tuzo hiyo imekabidhiwa pia kwa wanachama mbalimbali wa TAWLA katika mkutano mkuu wa mwaka wa 33 wa TAWLA uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam Mei 6,2023.
……………………………………….
JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejikita katika kupitia upya mifumo ya utoaji haki iliyopo ambayo imechangia kuvuruga mifumo ya haki jinai na kupuuza mifumo ya maadili na kusababisha baadhi ya wananchi wasio na uwezo kiuchumi kupoteza haki zao.
Akisoma Hotuba katika Mkutano wa Chama Cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) leo tarehe 6/5/2023 Jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa serikali iliamua kuanzisha tume ya muda mfupi ya haki jinai ambayo imelenga kuboresha taasisi za haki jinai na kutoa fursa kwa wadau kuchangia maoni.
Dkt. Ackson amesema kuwa serikali inaendelea ujenzi wa Vituo Jumuishi vya utoaji wa haki, huku akibainisha kuwa wamewahimiza majaji na mahakimu kuharakisha usikilizaji wa mashauri ili kuongeza kasi ya utoaji haki nchini.
“Nimefurahi kusikia miongoni mwa malengo ya TAWLA ni kuwasaidia wanasheria kujiendeleza kitaalama ili kuwasaidia wanawake wenye matatizo ya kisheria kwa ajili ya kupata haki zao” amesema Dkt. Ackson.
Amewapongeza uongozi wa TAWLA, Wafanyakazi pamoja na wanachama wote kwa kujitoa kwa moyo thabiti katika kutoa huduma ya kisheria kwa wanawake na watoto.
“Mmekuwa mkitoa msaada wa kisheria, kuelimisha jamii kuhusu haki za kisheria kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na kutetea haki za binadama, ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya wanawake na nchi kwa ujumla” amesema Dkt. Ackson
Dkt. Ackson alikuwa anamwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia katika mkutano huo, amesema kuwa TAWLA wamekuwa wakitoa huduma katika mikoa sita nchini jambo ambalo la kupongezwa kwani inaonesha nia ya dhati pamoja na kuhakikisha wanawafikia wanawake wa mikoa ya mbali ili wapate msaada wa kisheria.
Amesema wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwa serikali ikiwemo ushiriki wao katika kutunga sheria ya mtoto namba 21 mwaka 2009 ambayo inalinda haki na usawa wa watoto.
“Mmeshiriki katika mchakato wa kupata Katiba mpya kwa kuhakikisha katiba inayoandiwa inalinda haki za kijinsia” amesema Dkt. Ackson.
Hata hivyo amewataka kila kiongozi na mwanachama wa TAWLA kufanya juhudi za kutafuta na kufikia usawa kijinsia pamoja uwezeshaji kwa wanawake.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wanasheria wanawake Tanzania (TAWLA) Lulu Ng’wanakilala, amesema kwa kipindi cha miaka 33 TAWLA wameweza kuwatumia mawakili wake zaidi ya 400 kwa kuwasaidia wanawake mahakamani ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za mawakili.
Ng’wanakilala amesema kuwa lengo ni kutoa huduma kila Mkoa hivyo ametumia fursa hiyo kumuomba Rais Dkt. Samia kuwapa maeneo ya kujenga Ofisi ili waweze kuwafikia wanawake wenye uhitaji wa msaada wa kisheria.
“Tumeweza kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake milioni 12 kupitia Ofisi zetu zilizopo Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza na Dodoma” amesema
Ng’wanakilala.
Amesema ili kuwafikia watu wengi wamezindua huduma ya kutoa msaada wa kisheria kwa njia ya simu bila malipo pamoja na kuandaa mafunzo na machapisho kupitia vyombo vya habari na kufanikiwa kuwafikia watu milioni 17.
Amesema wamekuwa mstali wa mbele katika kutetea mabadiliko ya sheria mbalimbali kandamizi na kuhamasisha kutungwa kwa sheria zinazowalinda wanawake na watoto na kuimarisha usawa wa kijinsia.
Hata hivyo amebainisha kuwa Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kujifunza mbinu bora kuhusu usawa wa kijinsia, kuzingatia usawa ili kuongeza upatikanaji wa haki kwa wanawake’
Kila mwaka mwezi mei TAWLA
wanakuwa na mkutano mkuu ambao unatanguliwa na mafunzo ya sheria ambayo yana lengo la kuwasaidia wanawake kukua kitaaluma.
Kupitia mkutano mkuu baadhi ya wanawake wamepata Tuzo ya Wanawake Wanasheria Vinara kwa wanawake ambao wamekuwa chachu ya kuleta maendeleo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa 33 wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania TAWLA uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam Mei 6,2023.
Naibu Waziri wa Wizara ya Sheria na Katiba Pauline Gekul akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama hicho Bi. Tike Mwambipile akifafanua jambo katika mkutano Mkuu wa 33 wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania TAWLA unaofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam Jumamosi Mei 6,2023.
Jaji Winfrida Beatrice Korosso akitoa mada katika mkutano mkuu huo wa mwaka wa Chama cha Wawasheria Wanawake Tanzania TAWLA uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWLA, Bi. Lulu Ng‘wanakilala akizungumza katika mkutano Mkuu wa 33 wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania TAWLA unaofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam Jumamosi Mei 6,2023.
Picha mbalimbali zikionesha wanachama wa TAWLA wakishiriki katika mkutano huo.
Picha ya Pamoja.