NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ipo katika mpango wa kuongezea bajeti kwa Taasisi ya Watumishi Housing Investment (WHI) kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kujenga nyumba za watumishi wa umma kila Mkoa jambo ambalo litasaidia watumishi kuishi katika makazi bora kwa kupangishwa au kununua kwa gharama nafuu.
Akizungumza leo tarehe 6/5/2023 Jijini Dar es Salaam wakati akifanya ziara katika mradi wa Nyumba za Mkazi Magomeni (Watumishi House), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amesema kuwa watumishi wa umma wakiishi katika makazi bora, karibu na eneo la kazi kunaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Simbachawene amesema kuwa lengo la serikali ni kuisaidia WHI ili kufikia malengo ya kujenga nyumba za watumishi wa umma na kuzimiliki au kupangishwa kwa gharama nafuu.
“Lengo ni kuongeza nguvu ili kuhakikisha Watumishi Housing Investment wanatimiza jukumu lake la kujenga nyumba kwa gharama nafuu ambazo zitapangishwa au kununuliwa na watumishi wa umma” amesema Mhe. Simbachawene.
Amesema kuwa WHI bado wanajukumu kubwa la kujenga nyumba kila Mkoa kwa sababu uhitaji wa nyumba kwa watumishi wa umma ni mkubwa na nyumba zilizopo ni chache.
“Tungependa kuona mfano mzuri hasa maeneo ya vijijini wanajenga nyumba za gharama nafuu ili mwalimu aweze kuishi kwa kununua au kupangishwa kutokana WHI ambao ni sehemu ya majukumu yao” Mhe. Simbachawene.
Amewapongeza WHI kwa kutekeleza majukumu yake kwa vitendo ndani ya muda mfupi kutokana taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2013 na kuanza kazi rasmi mwaka 2014 na kufanikisha kujenga nyumba za watumishi zaidi ya 900 mpaka sasa katika mikoa mbalimbali nchini.
Amefafanua kuwa licha ya kuwa na mtaji mdogo lakini wameweza kufikia malengo ya kujenga nyumba za watumishi wa umma, huku akibainisha kuwa mikakati iliyopo ni kuendelea kuwashirikisha wadau ikiwemo mifuko ya hifadhi ya jamii.
Mhe. Simbachawene ameeleza kuwa WHI wamekuwa wabunifu kutokana wameanzisha mfuko wa Faida Fund ambao umewakalibisha wadau mbalimbali nchini kuwekeza na mpaka sasa mfuko huo una mtaji wa bilioni 12.7 na kufikia thamani ya bilioni 15.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Watumishi Housing Investment (WHI) Dkt. Fredy Msemwa, amesema kuwa ziara ya Waziri Mhe. Simbachawene kwa ajili ya kuona ndani ya Wizara yake WHI inafanya nini ? ambapo leo amepata fursa ya kuzungumza na uongozi wa kila idara.
Dkt. Msemwa amesema kuwa lengo ni serikali ni kuona tunawafikia watumishi wa umma katika maeneo mbalimbali nchini jambo ambalo linaitaji tuwe na fedha ili kufikia malengo.
“Serikali imeanza kuchukua hatua ikiwemo kuiwezesha watumishi Housing ili iwe na mtaji mkubwa wa kujenga nyumba nyingi” amesema Dkt. Msemwa.
Amesema kuwa pia kuna mfuko wa uwekeza wa pamoja (Faida Fund) ambao unawalenga watanzania wote ambao wana nia ya kuwekeza na kukuza mitaji yao ambapo mfuko huo ulianza rasmi January 2023.
Ameeleza kuwa mfuko huo umefikisha bilioni 15 na thamani ya vipande imeongezeka kutoka Sh. 100 hadi kufikia Sh. 103. 42 hivyo ni ukuaji mzuri na mpaka kufikia mwisho wa mwaka huu upo uwezekano wa kufikia ukuaji wa asilimia 10 au 12.
Dkt. Msemwa amesema kuwa kwa sasa wanaendelea na utekelezaji wa mradi wa nyumba 1,000 Mkoani Dodoma, ambapo nyumba 203 tayari zimekamilika na Mkoa wa Dar es Salaam mwezi July mwaka huu wanatarajia kuanza mradi wa Kawe ambao utakuwa na nyumba 560.
“Tunaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi wa kujenga nyumba kwa gharama kwa nafuu kwa ajili ya Watumishi wa umma” amesema Dkt. Msemwa.