Na. Abel Paul wa Jeshi la Polisi-Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Nchini Tanzania limesema kuwa limeona mjadala katika mitandao
ya kijamii ikuhusiana na kifo cha Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma Bi.
Nusura Hassan Abdallah kilichotokea huko Mkoani Kilimanjaro.
Akitoa taarifa hiyo leo mei 06,20223 msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini kamishina
msaidizi mwandamizi wa Polisi David Misime amesema kuwa taarifa hizo
zimekuwa zikihusisha kifo hicho na ajali iliyotokea Jijini Dodoma aprili 26,2023
ikimhusisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi (Afya) Mhe.Dkt. Festo
Dugange ambapo zinadaiwa zimetokana na kipigo kutoka kwa mpenzi wake.
Msemaji wa Jeshi hilo amebainisha kuwa Jeshi la Polisi Tanzania lingependa kutoa
ufafanuzi kuwa, Polisi Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kuona taarifa hizo kupitia
mitandao ya kijamii na sababu zinazotolewa,wameshaanza uchunguzi kwa watu
mbalimbali,hospitalini alikotibiwa binti huyo ambapo amesema wanashirikisha
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali,Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na
wadau wengine wa haki jinai.
Aidha Jeshi hilo limetoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zilizosahihi na
zenye ukweli asisite kutoa taarifa hizo ili kuharakisha uchunguzi wa tukio hilo.
Pia SACP Misime amesema kuwa Jeshi la Polisi Nchini linasisitiza kuwa
Uchunguzi wa tukio hilo ukikamilika taarifa kamili ya kilichobainika kitatolewa
kwa umma na kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu za Nchi.