Wasimamizi na madereva wa kemikali wakiwa kwenye mafunzo .
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi na madereva wa kemikali Kanda ya Ziwa
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala mwenye suti (mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na wasimamizi na madereva wa kemikali Kanda ya ziwa
……..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wasimamizi wa kemikali katika maeneo ya migodini,viwandani,wauzaji na madereva wanaosafirisha kemikali wametakiwa kufuata taratibu,sheria pamoja na kutumia vifaa kinga wakati wa shughuli zao ili kuepuka madhara yake.
Akifungua mafunzo ya siku mbili leo Alhamisi Mei 4, 2023 ya usimamizi salama wa kemikali yaliyojumuisha Mikoa ya kanda ya ziwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala, amesema pamoja na kuwa na kemikali ambazo zinafaida nyingi katika shughuli za kila siku pia kemikali zinaweza kuleta madhara makubwa kwa afya na mazingira endapo hazitatumika katika hali ya usalama ikiwemo kutokuvaa barako na vikinga mkono (groves).
Amesema umuhimu wa mafunzo hayo ni kuhakisha wanapata uwezo wa usimamizi salama wa kemikali ili kulinda afya za watu na mazingira dhidi ya madhara yatokanayo na kemikali zinazosafirishwa.
Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya ziwa Mussa Kuzumila, amesema lengo la mafunzo ni kutoa uelewa wanamna ambavyo kemikali zinapaswa kusimamiwa katika usahihi kwa lengo la kulinda afya za watu na mazingira.
Amesema mafunzo hayo kwa kanda ya ziwa ni ya nne na wanatarajia kupata mabadiliko chanya kwa wadau wa kemikali.
Kuzumila amesema kuna aina mbalimbali za kemikali ikiwemo hatarishi na zisizohararishi hivyo kunaathari nyingi ambazo zinaweza kujitokeza endapo dereva hatakuwa na uelewa wa kusafirisha kemikali hatarishi kwani inaweza kuleta madhara makubwa kwenye jamii.
“Dereva anapokuwa amebeba kemikali hatarishi anapaswa aende mwendo mdogo mdogo na akae katika sehemu ambayo haina mkusanyiko wa watu hatua itakayosaidia kuepusha ajali zisizokuwa za lazima”, amesema Kuzumila
Kwa upande wake mmoja wa madereva wa magari ya masafa marefu yanayosafirisha kemikali Mkoani Geita, Emmanuel Makindi amesema mafunzo hayo yamemuongezea wigo mpana wa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu sanjari na kuwashauri madereva kuacha tabia ya kutumia kilevi wakiwa kazini.