Mwandishi: Shabani Shabani
Barua pepe: [email protected]
Ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo nchini China kuanzia tarehe 17-28 Aprili 2023 inatukumbusha msemo wa waswahili usemao “Mguu wa kutoka una baraka”. ziara hii ya Kimkakati ambapo Katibu Mkuu wa CCM aliambatana na Wajumbe kumi na mbili (12) wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambao ni Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wajumbe watano (5) wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na Maafisa wa Chama pamoja na mambo mengine Taifa letu limevuna faida nyingi sana ambazo kila Mtanzania anapaswa kujivunia na kuwa tayari kuzitumia.
Yafuatayo ni mambo matatu yenye faida yatokanayo na ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Nchini China.
Mosi, Wawekezaji Tanzania: Tarehe 23 Aprili, 2023 Katibu Mkuu wa CCM na Ujumbe walikutana na Kampuni ya Sinotruck, Kampuni hii ndio kampuni ya kwanza kuzalisha magari yenye uzito mkubwa nchini China ambayo ilitajwa na jalida la Forbes kama kampuni namba 192 kati ya kampuni 2000 kubwa zaidi ulimwenguni kwa mwaka 2019, kampuni ambayo ina masoko katika mataifa 90 ulimwenguni na yenye wastani wa kuuza jumla ya magari 5000 kwa kila mwezi.
Kampuni ambayo mtaji wake umeongezeka kutoka kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 487.3 kwa mwaka 2020 hadi kufikia kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 668.2 kwa mwaka 2020, huku mapato yake kwa mwaka yakiongezeka kutoka kiasi cha Dola za kimarekani Bilioni 98 kwa mwaka 2020 hadi kufikia Dola za kimarekani Bilioni 14.5 kwa mwaka 2022.
Taarifa rasmi ilitolewa na kampuni ya Sinotruck imethibitisha kuwa wameanza ujenzi wa kiwanda cha kampuni yao nchini Tanzania huku wakiahidi kuhakikisha ujenzi unakamilika mwaka huu ili kampuni hii ianze kuzalisha malori. Hii ni faida kubwa sana kwasababu itakwenda kutoa fursa nyingi kwa Watanzania hususani ajira na itachochea ukuaji wa uchumi kwa Taifa letu kutokana na mapato yatakayokusanywa wakati wa uendeshaji wa kampuni hii na hata wakati wa mauzo ya bidhaa zao.
Siku hiyo hiyo ya tarehe 23 Aprili 2023 Katibu Mkuu wa CCM alifanikiwa kukutana na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Huajin Group ambayo inajihusisha na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za ngozi. Kampuni hii ambayo mwaka 2006 ilipewa mtaji wa Dola Bilioni 1 na benki ya maendeleo ya China inatajwa kuwa miongoni mwa makampuni makubwa yanayofanya vizuri sana kimataifa kutokana na uhakika wa kusambaza bidhaa zake zenye thamani ya Dola za kimarekani Milioni 1 katika mataifa ya Uingereza na Marekani kwa kila mwezi.
Aidha, kampuni hii ya Huajin Group ilianza uwekezaji wake wenye thamani ya Dola za kimarekani Bilioni 2 katika nchi ya Ethiopia tangu mwaka 2012. Licha ya Kampuni hii kuajiri watu 100,000 katika nchi hii ya Ethiopia lakini imekuwa na mchango mkubwa katika Taifa hili kwasababu ya utamaduni wake wa kuhakikisha inasaidia wafanyakazi wote wanaotokea katika familia duni.
Ni wazi kwamba Katibu Mkuu wa CCM kufanikiwa kutembelea na kuzungumza na uongozi wa kampuni hizi mbili zenye mitaji mikubwa sana pamoja na uhakika wa masoko kwa Mataifa makubwa ulimwenguni ni hatua kubwa sana ambayo italeta fursa nyingi sana kwa Watanzania, ikiongeza kujiamini kwa wawekezaji hawa ambapo uwekezaji wao utachochea ukuaji wa uchumi kwa Taifa letu kupitia kodi na vyanzo vingine vya mapato vitakavyotokana na uendeshaji wa kampuni hizi ikiwemo ajira zitakazozalishwa na kampuni hizi.
Pili, Lugha ya Kiswahili: Tanzania imebarikiwa utajiri wa lugha nzuri ya kiswahili na ya kipekee inayokua na kuenea kwa kasi kubwa sana hata kufikia hatua ya Umoja wa Mataifa kuitangaza siku ya tarehe 7 Julai kuwa ni silku maalumu ambayo dunia inaadhimisha lugha ya kiswahili, hivyo tayari zipo juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha lugha hii inaendelea kukua ambapo tayari sera mpya ya mambo ya nje ya Nchi imeipa kipaumbele lugha ya Kiswahili.
Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM nchini China imeacha alama kubwa sana inayothibitisha kwa vitendo namna lugha ya Kiswahili inavyopewa kipaumbele kikubwa na Chama na Serikali. Hii inatokana na lugha ya Kiswahili kutumiwa kwa mara ya kwanza na Katibu Mkuu wa CCM katika Ukumbi wa Mikutano wa Great Hall of the People of China tangu ukumbi huu ulipoanzishwa na kutumika kupokea na kufanyia mazungumzo na Viongozi kutoka katika Mataifa mbalimbali ulimwenguni tangu mwaka 1959, kwa mara ya kwanza kiswahili kimetumika katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM katika ukumbi huu alifanya hivyo wakati alipokutana na Mkurugenzi wa Kamisheni ya Mambo ya Nje ya Chama cha Kikomunisti cha China Ndugu Wang YI.
Tatu, Watanzania China; Katika ziara yake Katibu Mkuu wa CCM na ujumbe wake wamekutana na Watanzania waishio na wanaofanya shughuli zao China hasa za kibiashara na masomo ambapo amewahakikishia kuwa Serikali ya CCM ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa shughuli za watanzania za kibiashara kati ya China na Tanzania zinafanyika vizuri na zinafanikiwa, ambapo Ubalozi mdogo wa Tanzania Nchini China umeanzisha kipindi cha elimu kwa umma ambacho kitawasaidia watanzania kufahamu mbalimbali ya fursa na teknolojia.
“Nitoe rai kwenu ndugu zangu mliopo mstari wa mbele hapa China, kuongeza jitihada za kuvutia teknolojia na mitaji sambamba na kuchangamkia masoko ya bidhaa ambazo ndugu zetu hawa wametufungulia njia. Shirikianeni ili kuongeza nguvu ya kunufaika na fursa hizi za China. Waswahili wanasema kidole kimoja hakivunji chawa. Lazima kushikamana na kushirikiana ili kunufaika. Hapa kuna fursa kwa kila mmoja. Tusiweke mbele ubinafsi, umimi na roho ya kwanini apate.” Alisisitiza Ndugu Chongolo
Huu ni muendelezo wa ziara za kimkakati za Chama Cha Mapinduzi zenye maslahi mapana ya CCM na Watanzania kwa ujumla.