Mchungaji wa Kanisa la Moravian Usharika wa Singida Mjini, Yona Mbogo, akiwaombea Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mwenge wanaotarajia kufanya mitihani yao ya mwisho hivi karibuni wakati akihubiri ibada ya Jumapili iliyofanyika leo Aprili 30, 2023 katika Kanisa Kuu la Moravian Singida liliopo eneo la Mwenge Manispaa ya Singida
Na Dotto Mwaibale, Singida
MCHUNGAJI wa Kanisa la Moravian Usharika wa Singida Mjini, Yona Mbogo amesema njia
pekee ya kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili ukiwamo ushoga na
usagaji ni kumtegemea Mungu lakini kuwakamata na kuwaweka gerezani
wanaojihusisha na vitendo hivyo ni kuongeza ukubwa wa changamoto hiyo.
Mchungaji Mbogo ameyasema hayo wakati akihubiri ibada ya Jumapili
iliyofanyika leo Aprili 30, 2023 katika Kanisa Kuu la Moravian Singida liliopo
eneo la Mwenge Manispaa ya Singida ibada ambayo somo lake kubwa lilihusu
umuhimu wa utoaji wa zaka .
“Jambo hili la mapenzi ya jinsia moja ni pana hivi mfano unapowakamata
wanaojihusisha na vitendo hivyo unakwenda kuwaweka gereza gani kwasababu hivi
vitendo vinafanywa kati ya mwanaume na mwanaume, mwanamke dhidi ya
mwanamke,” alihoji Mchungaji Mbogo.
Alisema kutokana na mazingira ya jambo hili yalivyo njia pekee inayoweza
kusaidia kukabiliana na vitendo hivyo ni jamii kuendelea kuzingatia masuala ya
maadili kuanzia ngazi za familia na kumtumainia Mungu atuepushe na janga hilo.
Alisema kuporomoka kwa uchumi wa kipato kwa jamii ndiko kumetoa mwanya kwa
baadhi ya wafadhili kupenyeza fedha kupitia Taasisi zisizo za kiserikali
(NG’OS) na watu binafsi ambazo zimekuwa zikitumika kuhamasisha vitendo hivyo.
Akizungumzia suala la utoaji wa sadaka na zaka alisema ni jambo kubwa
katika imani kwani mtu anayemtolea Mungu zaka kwa ukamilifu umuongezea mara
dufu tofauti na yule anayekuwa mwizi wa kumuibia zaka hiyo kwa kutoa chache tofauti na ile
aliyojaliwa kama alivyofanya Anania na mke wake Safina waliotajwa katika biblia
ambao walishindwa kutoa zaka yao kwa ukamilifu kutokana na udanganyifu.
Alisema Mungu amehimiza kutolewa zaka asilimia 10 kutoka mapato ya kila
kitu kinachopatikana iwe mshahara, mazao, mifugo na vinginevyo.
Alisema mtu anapotoa zaka kwa uaminifu Mungu anatengeneza agano kati yake pamoja
na kizazi chake chote akimtolea mfano Abrahamu jinsi alivyo barikiwa baada ya
kutoa kwa unyenyekevu na uaminifu akawa tajiri mkubwa.
Aidha, Mchungaji Mbogo alisema kutoa zaka kwa Mungu isiyo kamili ina leta
laana kwa vizazi hadi vizazi na
kusabisha mtu kupata matokeo mabaya ya
maisha yake ikiwemo mikosi kama kufukuzwa kazi, kufeli masomo, magonjwa,
biashara kudorora, kupata fedha lakini zinapotea pasipo ya sababu kutokana na
matumizi yasiyofahamika na mengine mengi yanayofanana na hayo hadi kufikia
hatua akidhani amerogwa.
Alisema mtu akishindwa kutoa sadaka ya Sh.500 hata akipata Sh.Milioni 1
hata weza kutoa hivyo aliwaomba waumini wa kanisa hilo kujenga tabia ya
kumtolea Mungu sadada na zaka na Mungu atawabariki na vizazi vyao.
Mchungaji Mbogo akizungumzia umuhimu wa kwenda kusali alisema kuna watu
wamekuwa wakichelewa kwenda ibadani kwa kutoa visingizio mbalimbali vikiwemo
sikuwa na nauli au mtoto alikuwa mgonjwa na vingine vingi lakini mtu huyo huyo
anapokuwa na jambo lake la kupata fedha kama kwenda kwenye vikoba yupo tayari
kukodi hadi bodaboda ili afike haraka.
“Jambo hili sio zuri na halimpendezi Mwenyezi Mungu nawaombeni
wakristo kujenga tabia ya kuwahi kufika kanisani mapema tuacheni tabia ya kuwa
na sababu mbalimbali” alisema Mchungaji Mbogo.
Katika ibada hiyo Mchungaji Mbogo alifanya maombi maalumu ya kuwaombea
Wanafunzi wa Sekondari ya Mwenge ambao wanatarajia kufanya mitihani yao ya
mwisho hivi karibuni.