Na. WAF – Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kwamba katika kila vizazi hai 160 mtoto mmoja huzaliwa na tatizo la Usonji Tanzania.
Waziri Ummy ameyasema leo aliposhiriki Marathon ya kuchangia huduma za Usonji zilizofanyika katika viwanja vya Green Garden-Oysterbay Jijini Dar es Salaam.
“Lakini takwimu za sasa kwenye vituo vya huduma za afya na shuleni zinaonesha kuwa takribani watoto 2000 tu ndio wanaopatiwa huduma.” amesema Waziri Ummy
Aidha, amesema ukilinganisha na hali ya uzazi nchini ambapo jumla ya wanawake milioni 2.4 hujifungua kila mwaka na kwa makadirio ya WHO inaonesha kuwa kila mwaka watoto zaidi ya 15,000 huzaliwa na tatizo la Usonji kwa kiwango tofauti.
Akielezea tatizo la Usonji Waziri Ummy amesema kuwa Usonji ni tatizo la kibaiolojia ambalo humkumba mtoto akiwa ndani ya tumbo la mama yake na tatizo hilo hujidhihirisha zaidi mtoto anapofikia umri wa miaka mitatu.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema katika kukabiliana na tatizo la idadi ndogo ya walimu, shule chache zenye uwezo wa kuhudumia watoto wenye mahitaji maalum, Serikali imeanzisha mafunzo ya ngazi ya stashahada (diploma) katika Chuo cha Ualimu Patandi Arusha na vyuo vikuu vingine.
Sambamba na hilo, Waziri Ummy amebainisha kuwa Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo Wizara ya Afya imeimarisha huduma za Afya ya Akili pamoja na Huduma za Utengamao ili kuweza kuongeza ufanisi kwenye huduma hizo.
Mwisho, Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya inashirikiana na Sekta nyingine muhimu ikiwemo Sekta ya Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu eneo linaloshughulikia watu wenye ulemavu, Wizara inayoshughulikia masuala ya Maendeleo ya Jamii, wanawake na makundi maalum pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha kuwa wanashirikiana ili kuleta tija katika upatikanaji wa huduma hizi.