Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizindua vifaa vya shamba, uchimbaji wa visima virefu, ngombe wazazi na uvunaji wa malisho vyenye jumla ya zaidi ya shiling bilioni 4.6 ikiwa ni uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha Ranchi za Serikali.
Tukio hilo limefanyika Aprili 27, 2023 katika Ranchi ya Taifa ya Kongwa iliyopo mkoani Dodoma.
…………………………….
Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuonesha dhamira yake ya kuhakikisha sekta za uzalishaji zinasaidia kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja.
Hayo yamesemwa jana Aprili 27, 2023 katika Ranchi ya Kongwa mkoani Dodoma, wakati Waziri wa Mifugo, Mhe. Abdallah Ulega akikagua vifaa vya malisho, visima virefu, ng’ombe 1000 na shamba la malisho ya mifugo ikiwa ni uwekezaji uliofanywa na Serikali.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa azma yake ya kubadilisha na kuboresha sekta ya mifugo nchini na leo sote tumeshuhudia ambavyo Serikali yake imenunua vifaa hivi vyenye lengo la kusaidia katika uzalishaji wa malisho ya mifugo”. Alisema Waziri Ulega.
Alisisitiza “Kipaumbele chetu katika mwaka huu ni malisho ya mifugo hivyo ni jambo jema tumepata vifaa hivi vya kisasa vya kuvuna majani. Hili shamba la NARCO kwa maelekezo ya Mhe. Rais ni la mfano, lengo letu ni kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya mifugo”.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa, Prof. Peter Msoffe alisema kuwa Serikali imefanya uwekezaji huo kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya mifugo nchini ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali ilitenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kuboresha ranchi ya Kongwa iliyopo Dodoma na Mzeri iliyopo mkoani Tanga na maboresho haya yatafanyika katika ranchi zote 15 nchini isipokuwa kwa sasa tumeanza na hizi mbili”. Alisema Prof. Msoffe.
Aidha, Prof. Msoffe alifafanuwa “Maboresho yaliyofanyika ni uchimbaji wa visima virefu, ununuzi vifaa vya shamba ambavyo ni matrekta mapya manne, mashine za kukata majani tatu, reki saba, mashine za kufunga marobota ya nyasi nne, ng’ombe 1000 na uvunaji wa malisho katika ranchi ya Kongwa ambapo jumla ya gharama za maboresho hayo ni zaidi ya shilingi bilioni 4.