Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso (Mb) amekutana na wakandarasi wanaotekeleza mradi wa maji wa Miji 28 na kuwaeleza kuhusu ubora unaotarajiwa katika ujenzi.
Mradi huo ni moja ya mradi mkubwa wa maji wa kimkakati hapa nchini na unafanikishwa na Serikali kupitia mkopo nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim ya India.
Waziri Aweso amewatakia kheri wakandarasi hao katika utekelezaji wa kazi hiyo muhimu ya kuwapatia Watanzania huduma ya majisafi.
Amewataka wakandarasi kufanya kazi kwa nguvu kubwa kwa sababu mradi huo umesubiriwa muda mrefu.
Waziri Aweso amewaeleza kuhusu matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye alishuhudia utiaji saini wa mradi katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Utekelezaji wa mradi wa maji wa Miji 28 ulianza tarehe 12 Aprili, 2022 baada ya serikali kukamilisha taratibu za masuala ya kodi na kulipa malipo ya awali (Advance payment) kwa wakandarasi ambao sasa hivi wametawanyika katika maeneo yaliyo katika mpango na kazi imeanza.
Mradi huu utanufaisha miji ya Kaliuwa, Sikonge, Urambo, Kasulu, Mpanda,Kilwa Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Rujewa, Makambako, Njombe, Wangingombe, Chunya,Chamwino, Chemba, Singida, Manyoni, Mugumu, Geita, Kayanga, Chato, Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani, Mafinga, Songea, Rorya / Tarime, na Makonde.