Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer ameipongeza kampuni ya Franone Mining LTD kwa kuwapatia shilingi milioni 30 za ujenzi wa ukumbi wa chama hicho.
Kiria ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Miningi LTD, Onesmo Mbise walipokutana kwenye kijiji cha Naepo kata ya Naisinyai.
Amesema kitendo cha kampuni hiyo kuchangia shilingi milioni 30 za ujenzi wa ukumbi wa chama hicho kinastahili pongezi kubwa kwani wameonyesha moyo wa upendo kwa CCM.
“Kwa niaba ya CCM Wilaya ya Simanjiro, pokea salamu za asante na ninakushukuru kwa kutuunga mkono katika ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa chama chetu,” amesema Kiria.
Amesema mkurugenzi huyo ameonyesha mfano mkubwa kwa wawekezaji waliopo kwenye wilaya ya Simanjiro katika kukiunga mkono chama hicho hivyo anastahili pongezi.
Pia, Kiria amempongeza mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite bilionea Saniniu Laizer na mwekezaji mwingine God Mwanga (Charity) kwa kuchangia ujenzi wa ukumbi huo wa chama.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Franone mining LTD, Onesmo Mbise amemuhakikishia Mwenyekiti huyo wa CCM wa Wilaya ya Simanjiro Kiria Laizer kuendeleza ushirikiano uliopo.
“CCM ndiyo chama ambacho kinaisimamia Serikalli ya awamu ya sita hivyo siyo vyema chama hiki ngazi ya wilaya kukosa ukumbi wa kukutana hivyo nawapongeza kwa hatua hiyo,” amesema Mbise.
Awali, chama hicho kilikuwa kinafanya mikutano na wanachama wake au uchaguzi kwenye kumbi za makanisa au shule ya sekondari Simanjiro kutokana na kukosa ukumbi.
Hivi sasa chama hicho kimeunda kamati ya ujenzi wa ukumbi inayoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera na katibu wake meneja wa RUWASA Wilaya ya Simanjiro mhandisi Joanes Martin.