Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise (katikati) akielezea baadhi ya miradi itakayotekelezwa na kampuni hiyo kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha sita ya shule ya sekondari Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kushoto ni Diwani wa Kata hiyo Taiko Laizer na Mkuu wa shule hiyo William Ombay.
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
KAMPUNI ya Franone Mining LTD inayochimba madini ya Tanzanite, imeahidi kufanikisha miundombinu ya thamani ya Sh38 milioni ya shule ya sekondari Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise ameyasema hayo akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha sita ya shule hiyo ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Mbise amesema watafanikisha changamoto hizo alizoahidi mara baada ya kukutana na wakurugenzi wenza wa kampuni hiyo, Vitus Ndakize na Francis Matunda.
Ametaja changamoto zitakazotatuliwa na kampuni hiyo ni kisima, umeme wa nyumba, bweni la wasichana na bwalo na jiko la kudumu kwani lililopo linaingiza vumbi na kuchafua chakula.
Hata hivyo, amesema taratibu na kanuni za kusaidia jamii iliyo pembeni ya uwekezaji (CSR) imebadilika hivi sasa kwani mkurugenzi wa halmashauri ndiye anapendekeza eneo tofauti na awali.
“Hivi sasa unaweza kuwekeza Naisinyai au Mirerani ila mkurugenzi wa halmashauri akachagua kata nyingine ya kutekeleza CSR ili mradi ipo Simanjiro,” amesema Mbise.
Amesema anawapongeza walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Naisinyai ambayo ni miongoni mwa shule za awali za kata wilayani Simanjiro zilizozalisha wasomi.
“Tunaipongeza serikali kwa kuanzisha shule za kata kwani zimesaidia watoto wa jamii ambao baadhi ya wazazi wasio na uwezo wanaweza kupata elimu ya sekondari,” amesema Mbise.
Mkuu wa shule ya sekondari Naisinyai, William Ombay amemshukuru Mbise kwa kupitia kampuni yake kuahidi kukamilisha baadhi ya changamoto zinazowakabili.
“Tunashukuru kwa ahadi za kusaidia shule yetu kwani serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kutimiza mahitaji ya shule ila wadau wa elimu kama ninyi siyo vibaya kusaidia pia,” amesema Mwalimu Ombay.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer amesema watampa ushirikiano wa kutosha mwekezaji mzawa Onesmo Mbise kupitia kampuni ya Franone Mining LTD inayochimba madini ya Tanzanite.
“Hii ni hatua nzuri ya mahusiano mema ya uwekezaji kupitia kampuni yako ya Franone Mining LTD na jamii ya kata ya Naisinyai, tunatarajia tutashirikiana vyema,” amesema Taiko