Na Dotto Mwaibale, Singida
WAFANYAKAZI wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa
Singida, wamefanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya ofisi yao
ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ambaye
alizitaka taasisi zote za Serikali mkoani hapa kufanya shughuli za usafi wa
mazingira ikiwa ni moja ya jambo muhimu kuadhimisha sherehe za miaka 59
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo kilele chake ni kesho Aprili 26,
2023.
Meneja wa NSSF) Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa akizungumza na waandishi wa habari mjini
hapa jana wakati wa zoezi la kufanya usafi alisema wanafanya usafi huo ikiwa ni
utekelezaji wa agizo la mkuu wa mkoa la kuzitaka taasisi zote za umma mkoani
hapa kufanya hivyo.
Alisema kufanya usafi ni jambo jema kwani unayafanya
mazingira ya ofisi kuwa mazuri na bora pia ni afya ambapo aliwataka watumishi
wa NSSF mkoani hapa kuendelea kufanya usafi wakati wote.
Akizungumzia kuhusu muungano wa Tanganyika na
Zanzibar alisema umetela amani na utulivu mkubwa katika pande zote mbili jambo
ambapo limechangia mfuko huo kuwa na mafanikio makubwa ya kuweza kuwalipa
wanachama wao kwa wakati na kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali hapa
nchini likiwepo daraja na Nyerere lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Kalimilwa aliwataka wananchi wa pande zote mbili
kuendelea kuwapongeza wahasisi wa muungano huo Rais wa kwanza wa Tanzania,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid
Amani Karume kwa kuanzisha muungao huo ambao umeleta tija kubwa na akatumia nafasi
hiyo kuwashukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Dk.Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar
kwa kuulinda muungano huo.
Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alizifuta
sherehe za miaka 59 ya Muungano na badala yake alitaka sherehe hizo kwa mwaka
huu zifanyike katika ngazi ya kimikoa kwa kufanya usafi wa mazingira na
shughuli zingine za kijamii na kiuchumi badala ya kufanyika kwa gwaride kama
ilivyozoeleka.
Meneja wa(NSSF) Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana wakati wa zoezi hilo la kufanya usafi.