Na John Walter-Manyara
Mrara Fc ya Mjini Babati imenyakua Kombe la Polisi Jamii Cup 2023 mkoani Manyara baada ya kuifunga Soldiers Boys ya wilayani Hanang’ mabao 2-0 katika fainali zilizopigwa uwanja wa Kwaraa mjini Babati.
Nyota wa mchezo ni kipa wa Mrara Fc Ramadhani Nyanda ambaye hakuruhusu bao hata moja, amekabidhiwa shilingi elfu 2 huku mwenyekiti wa UVCCM Babati mjini Magdalena Urono akimpatia elfu 30 ahadi aliyoitoa kwa kipa ambaye hataruhusu bao hata moja.
Aidha mwenyekiti huyo aliahidi kununua kila bao kwa shilingi elfu 10 ambayo imeenda kwa wafungaji wa Mrara Fc John Pengo aliyefunga dakika ya 41 na Aidan Haidari aliyefunga dakika ya 50.
Mshindi wa tatu ni Sanu Fc ya Mbulu iliyoshinda kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Magugu Rangers ya Babati.
Mbali na kukabidhiwa kombe, Mrara Fc pia walikabidhiwa jezi, mpira na shilingi laki saba taslimu na mgeni rasmi mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere.
Pia mdhamini wa mshindano hayo Mati Super brands Ltd kupitia kinywaji cha Tai Original, Paa kibabe wamekabidhi zawadi mbalimbali kwa timu zilizoshika nafasi ya pili na ya tatu.
Awali akizungumza katika mashindano hayo kamanda wa polisi mkoa wa Manyara George Katabazi amesema lengo la Polisi jamii ni kuimarisha mahusiano baina ya wananchi na Jeshi la Polisi jambo ambalo limefanikiwa.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amewataka wananchi wawe na tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuweka afya zao vizuri na kuepuka maradhi.
Viongozi wengine waliokuwepo uwanjani hapo kushuhudia faina hizo ni Pamoja na Mkuu wa wilaya ya Hanang’ Janeth Mayanja,Katibu tawala mkoa wa Manyara Carolina Mthapula na Mwenyekiti wa UVCCM Babati mjini Magdalena Urono.