Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mh. Mwanaidi Ali Hamis ametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha kulea watoto Hisani Orphanage Centre, kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt Joyce Nyoni ambaye amemuwakilisha Mh. Naibu Waziri, amewaasa watoto hao kutokata tamaa na kumuomba Mungu awape ujasiri, kusoma na kufanya kazi kwa bidii na pia kufuata utaratibu.
Aidha amesema kuwa Wizara inajitahidi kuhakikisha watoto wanalindwa na kuhakikisha ustawi wao.
“Wizara inajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunalinda watoto, tunahakikisha ustawi wao” amesema Dkt. Nyoni.
Baada ya kuzungumza na watoto katika kituo hicho kinacholea jumla ya watoto 71 ambao walijumuika na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mizimbini, kwa niaba ya Mh. Naibu Waziri, Dkt. Joyce Nyoni amekabidhi mahitaji muhimu kwa watoto katika kituo hicho.
Zawadi zilizotolewa ni pamoja na; Mchele, Sukari, Unga wa Sembe, Mafuta ya Kupikia , Maharage, Tambi,Sabuni za kufulia, Miswaki , Dawa za Meno, Mafuta Kupaka, na Sabuni za Kuogea