Na Beatrice Sanga-MAELEZO
TAASISI na Mashirika ya Umma yanayojiendesha kwa kutegemea mfuko wa Serikali Kuu yametakiwa kuhakikisha yanapunguza utegemezi wa rasilimali fedha na kuhakikisha kwamba yale yanayochangia kwenye Serikali yaendelee kuchangia kwa ufanisi zaidi, ili kuhakikisha kwamba uwekezaji uliofanywa na Serikali unaonekana kupitia uzalishaji wake.
Hayo yameelezwa Jijini Dar es Salaam Aprili 20, 2023 na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu wakati akifunga mkutano wa siku mbili kati yake na Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali, ambapo leo amekutana Mashirika na Taasisi zaidi ya 170 ambazo zinatoa huduma kwa jamii zilizo chini ya Ofisi yake.
Ameleza kuwa ofisi yake itahakikisha Mashirika na Taasisi zinazojihusisha na utoaji huduma zinaongeza tija katika uzalishaji na kuchangia pato la Taifa kutokana na shughuli wanazofanya kuliko kutegemea zaidi fedha kutoka mfuko wa hazina kwa ajili ya kujiendesha.
“Leo tulikuwa tunakumbushana wajibu, mipango iliyoko mbele na mategemeo yetu kutoka kwenye Taasisi hizo ili tuweze kuona kile ambacho wanakifanya kwa hiyo mojawapo ya vitu tunavyohitaji kwa wale ambao hawatengenezi faida tunahitaji basi wapunguze utegemezi kutoka kwenye serikali kuu,” na kuongeza,
“Huo ndo mchango wanaweza wakautoa kama huna uwezo wa kuchangia faida kwenye Serikali Kuu, wale ambao wanachangia tunataka waendelee kuchangia, lakini kuongeza ufanisi kikubwa ambacho tunataka uwekezaji ambao umefanywa na serikali kwenye taasisi yoyote tuwe na ufuatiliaji wa karibu kwamba maslahi yake yanaweza yakaonekana.”
Msajili huyo wa Hazina amesema kuwa ofisi yake, wakiwa ndo wasimamizi wakuu wa Taasisi na Mashirika hayo watahakikisha wanapunguza changamoto zinazokabili katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kubadilisha baadhi ya sheria pamoja na usimamizi mzuri wa kanuni na miongozo ili kuongeza tija kwa Mashirika na Taasisi hizo.
“Changamoto ambazo zilikuwepo na ambazo tunaziona ni zile zile zinazojirudia, moja ni kukokesana kwa maono ya muda mrefu, wanaosimamia Taasisi wana maono gani juu ya Taasisi, wanataka nini kifanyike, wanakwenda wapi, lakini ya pili ni kukosekana kwa usimamizi thabiti, kwa hiyo wajibu wa kuwawezesha kwa mtaji ni wetu, lakini wajibu wa kurekebisha sheria zinazowavunja miguu tunazifanyia kazi, kwa kweli umekuwa ni mkutano wenye manufaa.” Ameeleza Mchechu.
Lakini kwa upande wake, Prof. Sylvia Temu Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wakurugenzi ya Wahasibu na Wakaguzi, amesema kuwa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma zina wajibu wa kusimamia uendeshaji wa Mashirika na Taasisi ili kuongeza tija na uzalishaji katika Mashirika hayo, na pia amesema watafanyia kazi maelekezo na maono ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kuhakikisha kuwa wanaongeza uchangiaji wa pato katika mfuko wa Hazina.
“Msajili wa Hazina amesisitiza kwamba ipo haja ya mashirika ya umma kujitathmini kwa lengo la kuongeza mchango wake katika mfuko wa fedha wa kodi, sasa hivi mashirika yote ya umma tunachangia shilingi bilioni 800 tu kwa mwaka, lakini kwa mwaka huu inatarajiwa tuchangie angalau shilingi Trilion 1 na hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ambao umefanyika, na uwekezaji wake sasa hivi umefikia Trilioni 70 unaweza ukaona uchangiaji kwa njia ambayo siyo ya kodi bado ni mdogo sana”
Naye, Stephen Wassira, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere amesema kuna haja ya serikali kuja na mipango endelevu ili kuhakikisha kwamba Mashirika na Taasisi zinajikita katika kuongeza uzalishaji na mnyororo wa thamani kuliko kuwa na mipango ambayo inabadilika mara kwa mara.
“Mimi nafikiri kwa mawazo yangu tunapaswa tuwe na mambo ambayo ni endelevu siyo kila mtu anayekuja, anakuja na cha kwake halafu mwingine akija anafuta kile tunapata changamoto kidogo.”
Kwa sasa Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia taasisi na mashirika 298, wakati huo mashirika 35 yanajihusisha na biashara, ilhali Mashirika 213 yanajihusisha na utoaji wa huduma, na mpaka sasa Serikali imewekeza zaidi ya Sh. Trilioni 70 katika mashirika haya na imekuwa ikitegemea kupata gawio kutoka katika mashirika, ingawa kumekuwa na kulegelega katika kujiendesha huku mengine yakikabiliwa na ukosefu wa mitaji na kujiendesha kwa hasara.
Mkutano huo wa siku mbili umehitimishwa leo na Msajili wa Hazina katika Kituo cha Mikutano cha Kimatifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.