Wakati jamii kielekea katika sherehe za Sikukuu ya Eid-El-Fitri, Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake, Zanzibar (TAMWA Zanzibar) kinawasihi wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa kuhakikisha kwamba watoto hawatoki peke yao kwenda sikukuuni.
Takriban kila mwaka wakati wa sherehe za sikukuu ya Eid Hajj au Eid El Fitri huripotiwa matukio ya udhalilishaji kwa watoto katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, ikiwemo kupotea kwa watoto, kubakwa, kulawitiwa, kutoroshwa na matukio ya aina hiyo.
Hivyo ni vyema wazazi na walezi kuwakinga watoto wasikumbwe na vitendo vya udhalilishaji katika sehemu mbali mbali za viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya sherehe hizo.
Kwa vile watendaji wa vitendo vya udhalilishaji,wanabadilisha mbinu mpya kila siku, na kukua kwa teknolojia hasa mawasiliano ya simu na kimtandao, TAMWA-ZNZ inatoa wito kwa wazazi kutoa taarifa mapema pale wanapogundua hali isiyokuwa ya kawaida ya Watoto wao au watu wanaowatuhumu kufanya vitendo hivyo.
TAMWA, ZNZ inaiomba jamii kuacha tabia ya kumpa dhamana mtoto kuwa ndio kiongozi wa kundi la watoto wengine wadogo kwani kufanya hivyo kunapelekea udhibiti mdogo wa watoto katika viwanja vya starehe.
Takwimu zilizotolewa mapema mwaka huu na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaonesha kuwa jumla ya watoto 1, 173 waliathirika na vitendo vya udhalilishaji na ukatili mwaka 2022. Kwa mujibu wa taarifa hiyo jumla ya matukio 883 (asilimia 75%) ambayo yaliripotiwa ni kwa watoto wenye umri kati ya miaka 11 hadi 17, hivyo watoto wapo katika hatari zaidi ya kukumbwa na vitendo vya udhalilishaji na ukatili.
TAMWA Zanzibar tunawatakia wananchi wote nchini Eid El Fitri njema.