……………………
Sixmund J. Begashe
Wizara ya Maliasili na Utalii nchini kupitia Idara yake ya Mambokale, imeendelea na jitihada zake za kuboresha maeneo ya Malikale ili kuvutia Watalii zaidi kama sehemu ya mkakati wake wa kuhakikisha inavuka lengo la idadi ya watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025
Akifungua kikao cha Wataalam kuhusu Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe Bagamoyo, Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini Dkt. Christowaja Ntandu, amesema Mji wa Bagamoyo una utajiri mkubwa wa Urithi wa Malikale lakini bado Urithi huo haujatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi hivyo ni wakati muafaka sasa kuhakikisha maboresho yanafanywa ili uvutie watalii wengi kwenye Mji huo.
“Mji wa Bagamoyo ni Urithi muhimu kwa Historia na Utalii wetu, hivyo tumeona tukutane na wadau mbalimbali wa Malikale ili tupate uelewa wa pamoja wa namna ya Kuhifadhi na kuendeleza Mji huu” aliongeza Dkt. Ntandu
Dkt. Ntandu amewataka Wataalamu wa Malikale, wadau , wamiliki wa Majengo ya Kale na Magofu kushirikiana vyema na Serikali katika kuhakikisha wanaongeza kasi katika kuhifadhi vyema, kuboreshwa na kuyalinda maeneo ya Malikale.
Akizungumzia hatua inayochukuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ya kushirikisha wadau wa Malikale, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo Bw. Majid Mhina amesema mkakati huo unakwenda sasa kuongeza ufanisi wa uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Bagamoyo na kuchochea pato la Wananchi wa Mji huo.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dkt. Simon Mpyanga ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuamua kukaa chini na wadau mbalimbali kwani hatua hiyo inakwenda kuokoa majengo mengi ya Kale katika Mji wa Bagamoyo ambayo yapo mbioni kupotea.
Mbali na hilo, Dkt. Mpyanga ameishauri Wizara hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kushiriki katika kulinda Urithi huo adhimu na adimu nchini kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na Kijacho.