Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na vijana wakati wa bonanza la michezo katika wiki ya vijana lililofanyika Mkoani Lindi Oktoba 12, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi akizungumza wakati wa kongamano hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiangalia mchezo wa Bao walipokuwa wakishindana Mzee Said Masteti na Abdallah Makwela. (Wa nne kulia waliokaa) ni Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Ali Karume na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde. Mchezo huo wa Bao alipenda kuucheza Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Vijana kutoka Shule ya Lindi Sekondari na angaza wakiwa uwanjani wakicheza mpira wa pete wakati wa bonanza hilo.
Mchezaji wa timu ya Sekondari ya Lindi Mwalimu Said (wenye jezi ya bluu) akijaribu kuwatoka wachezaji wa Angaza wakati wa bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Lindi.
Sehemu ya vijana wakifuatailia mchezo wa mpira wa miguu utambulikao kama soka mara baada ya bonanza hilo kufunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama Oktoba 12, 2019.
Baadhi ya Viongozi pamoja na wakazi wa Lindi wakifuatilia michizo ambayo ilikuwa ikiendelea katika viwanja vya Shule ya lindi sekondari.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi kombe kwa Mshindi wa Kwanza wa Mchezo wa Bao Bw. Said Masteti ambao ulikuwa Mchezo unaopendwa na Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere. (Wa tatu kutoka kulia ni Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Ali Karume. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
…………………..
Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewamiza vijana nchini kutumia michezo ili kuimarisha amani, upendo na mshikamano.
Waziri Mhagama alitoa kauli hiyo wakati wa Bonanza la michezo kwa vijana lililofanyika katika shule ya Sekondari Lindi ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya vijana nchini kuelekea kilele cha mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2019 na Kumbukizi ya Miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bonanza hilo ambalo vijana walikusanyika kwa lengo la kushiriki katika michezo mbalimbali, Mheshimiwa Mhagama alieleza kuwa michezo imekuwa ikitumika kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha ushirikiano na kuwajengea vijana ari ya uzalendo.
“Kupitia michezo mnayofursa kama vijana kuendelea kuenzi falsafa za waasisi wa taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume ambao walikuwa wazalendo kwa taifa lao na waliimarisha muungano kwa maslahi ya watanzania wote,” alisema Mhagama
“Ni matumaini yangu kuwa kupitia michezo hii mtaendela kujikumbusha falsafa za waasisi hao kupitia michezo hii tunayoifungua leo kwa kuwa itatoa hamasa kwa vijana kupenda nchi yao na itajenga ari ya kuendeleza kuimarisha mshikamano kupitia michezo,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa michezo hiyo iliyowakutaisha vijana ikatumike kama sehemu ya kuwa na amani, uvumilivu na mshikamano.
“Vijana mnatakiwa kujenga taifa kwa vitendo vinavyodumisha amani, upendo na mshikamano kama ambavyo Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere alivyotujengea taifa lenye umoja,” alieleza Mhagama
Aidha Waziri Mhagama aliendelea kuwasihi vijana kutambua wajibu wao katika jamii na kuifanya michezo kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu wanayopaswa kuyaendeleza katika kutekeleza mipango waliyonayo.
Pamoja na hayo alirejea ujumbe wa Mwenge wa uhuru mwaka huu ambao pia umesisitiza ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa Serikali za Mtaa. Aliwaomba vijana kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika uchaguzi ili waweze kupata viongozi bora kwa maendeleo ya taifa.
Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo pia kuwapongeza wadau mbalimbali na vijana walioshiriki bonanza hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi alisema kuwa Bonanza hilo la michezo limejumuisha vijana kutoka sehemu mbalimbali ikiwa ni njia moja wapo ya kuwaendeleza vijana ili waweze kuimarika kiafya na kiakili.