Wajumbe wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakiwa katika mafunzo ya kupatiwa uelewa wa majukumu yao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tsrehe 17 hadi 18 ,Aprili 2023.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA akifuatilia kwa makini mafunzo ya wajumbe wa Bodi kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Dkt. Stephan Ngailo akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya wajumbe wa Bodi kuhusu wajibu wa Menejimenti katika kutekeleza dhima na Mpango Mkakati wa Taasisi .
…………………………..
Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imepatiwa mafunzo yanayolenga kuwaandaa kutekeleza majukimu yao mapya.
Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Chuo cha Uongozi yamefanyika jijijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 17 – 18, Aprili 2023.
Akiwasilisha mada kuhusu miongozo mbalimbali ya Ofisi ya Msajili wa Hazina inayosimamia Taasisi za Umma mtaalamu wa uchambuzi kazi
Bi.Rebecca Mahenge amesema wajumbe wa Bodi wanatakiwa kuifahamu miongozo hiyo katika kufanya maamuzi yao.
Bi Mahenge amesema kuwa baadhi ya miongozo ya kuwasaidia wajumbe wa bodi kufanya kazi zao kwa ufanisi ni pamoja na mwongozo wa utendaji wa wajumbe wa Bodi, mwongozo wa tathmini ya utendaji kazi wa Bodi na mwongozo unaoelezea mipaka ya kiutendaji kati ya Bodi na Menejimenti.
Akifungua mafunzo hayo awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA Dkt. Anthony Diallo aliwataka wajumbe wa Bodi kujielimisha na kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kuisimamia Taasisi hiyo kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu.
Dkt Diallo amesema kuwa ni muhimu wajumbe wakayafahamu majukumu yao vema ili waweze kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya taasisi.
Akiwasilisha mada kuhusu Utawala Bora mwezeshaji kutoka Chuo cha Uongozi Charles Senkondo amesema mapambano dhidi rushwa, matumizi sahihi ya rasilimali za taasisi na kutokutumia vibaya madaraka waliyopewa wajumbe ni nyenzo muhimu za kukuza utawala bora.
Senkondo amesema kuwa baadhi ya wajibu wa Wajumbe wa Bodi ni kusimamia masuala ya kimkakati ya Taasisi ili kufikia dhima iliyowekwa na Mamlaka.
Ameongeza kuwa, majukumu mengine ya Bodi ni pamoja na kufanya maamuzi yao kwa haki na kwa maslahi mapana ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Senkondo amesisitiza kuwa ni vema wajumbe wa Biodi wakajiepusha na maslahi binafsi na kutokuwa na mgongano wa maslahi wanaposimamia majukumu waliyopewa.