Na. WFA- Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameitaka Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe kujikita katika masuala ya kukuza Afya ya akili ikiwa ndiyo lengo mahususi la kuanzishwa hospitali hiyo.
Mhe. Ummy ametoa wito huo leo Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Ushauri ya Hospitali ambapo amesema kuwa Hospitali hiyo inatakiwa kuwa kituo mahiri cha masuala ya Afya ya akili nchini.
Akizungumza Mhe. Ummy amesema kituo hicho kitahusisha huduma za tiba ya akili, tafiti mbalimbali za maradhi hayo, mafunzo ya Afya za akili na kuhamasisha jamii kuwa na uelewa juu ya Afya ya akili.
“Bodi na wajumbe natamani Mirembe tuiite Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili, nawaachia mjadili na mniambie kama ni kubadilisha sheria mimi nipeleke kwenye baraza ijadiliwe”, amesisitiza Mhe. Ummy
Sambamba na hayo, amesema Afya ya akili ni moja wapo ya maradhi yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kila siku ikichangiwa na kurithi, matumizi ya dawa za kulevya, pombe, matatizo ya kisaikolojia na hali ngumu ya Maisha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Praxeda Swai amesema anamshukuru Mhe. Ummy kwa uteuzi huo na amehaidi kuleta matokeo chanya katika utendaji wao ili hospitali hiyo iwezekufikia malengo yake.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Paul Lawale amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha hali ya utoaji hudumu za Afya nchini ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za Afya za Akili katika hospitali hiyo.