Hayo yamesemwa na Mwakilishi Mkazi wa UNPD hapa nchini Bi. Christina Msisi alipotembelea maeneo ya misitu ya mazingira asilia na ranger post yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma Tanzania leo tarehe 18 Aprili 2023 Mkoani Iringa.
Amesema kuwa maeneo hayo ya misitu ni maeneo muhimu sana kwa ustawi wa ikolojia na hivyo ni vyema maeneo hayo yakatunzwa vyema na kutumika kwaajili ya Utalii ambapo itapelekea ukuaji wa uchumi.
Aliendelea kusema kuwa ametembelea na kujionea namna TFS inavyosimamia na kuendeleza miradi iliyofadhiliwa na UNDP katika maeneo mengi na hivyo kufanya shughuli za uhifadhi na utalii kuongezeka kwa kasi kubwa katika maeneo ya misitu kama ilivyo katika hifadhi mbalimbali zinazosimamiwa na TFS.
” Maeneo mengi ilifanyika miradi iliyofadhiliwa na UNPD na kwa TFS miradi imesimamiwa vizuri na kufanya shughuli za utalii kukua kwa haraka na hii imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na watalii wanaotembelea maeneo hayo kuwa rahisi.” Amesema Mwakilishi Mkazi wa UNPD
Ameongeza kuwa utangazaji wa vivutio vilivyopo ndio chachu kubwa katika kutangaza fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo ya misitu na itasaidia kuwavutia wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje nchi kutembelea hifadhi za misitu.
“Mjitahidi sana kuweka ” subtitles” ya lugha nyingine za kimataifa katika matangazo yanayotolewa ili kutangaza fursa za utalii katika maeneo mengi Duniani” Ameongeza Mwakilishi Mkazi wa UNPD
Hata hivyo ameendelea kusisitiza uwepo wa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali wa masuala ya uhifadhi na utalii, taasisi mbalimbali na wananchi wanaozunguka katika maeneo ya hifadhi ili kulinda rasilimali za misitu zilizopo.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS wakati wa ziara hiyo Mhifadhi Mwandamizi Someni Mteleka anayeshughulikia Utalii amesema kuwa TFS imeendelea kuboresha miundombinu katika maeneo ya uhifadhi ili kuwavutia wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza katika maeneo ya misitu.
Amesema kuwa kutokana na uboreshaji wa mazingira katika misitu ya hifadhi imesaidia kuongeza ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kutokana na utalii kutoka watalii 46,000 hadi watalii zaidi ya 200,000 kwa mwaka na hivyo kufanya makusanyo hayo kutoka milioni 300 hadi bilioni moja kwa mwaka.
Ameongeza kuwa pamoja uboreshaji wa miundombinu na ongezeko la watalii katika hifadhi za misitu , TFS imeendelea kuweka alama katika mipaka ya hifadhi ili kulinda maeneo hayo, kukaribisha wawekezaji, kuwa na mikakati ya kutangaza fursa za utalii zilizopo katika maeneo ya misitu na kuhakikisha kunakuwa na uelewa wa pamoja na ushirikiano katika masuala ya uhifadhi kati ya wadau, wananchi na taasisi mbalimbali .
Mwakilishi Mkazi wa UNPD ametembelea Msitu wa Hifadhi wa New Dabaga Ulogambi na Ofisi ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Kilombero.