Mdhamini wa Mshindano ya Tambaza Ramadhani Cup Imran Baba akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wachezaji wa mpira wa miguu wanaoshiriki Mashindano ya Tambaza Ramadhani Cup pamoja na viongozi wa CCM Kata ya Jangwani.
…………………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Michuano ya Tambaza Ramadhani Cup inayoshirikisha timu 10 kutoka Kata ya Jangwani leo tarehe 17/4/2023 imeendelea kutimua vumbi katika Uwanja wa fire uliopo Jijini Dar es Salaam ambayo imefika hatua ya nusu fainali.
Michuano hiyo inadhaminiwa na Mjumbe wa Kamati ya Michezo Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Bw. Imran N. Jaffer maarufu kwa Jina la Imran Baba, ambapo leo timu ya Mikumu imefanikiwa kutinga hatua ya Fainali baada ya kuichabanga Istanbul mabao mawili kwa moja.
Kesho tarehe 18/4/2023 michuano ya Tambaza Ramadhani Cup inatarajia kuendelea kwa mchezo mmoja wa nusu fainali ya pili kati ya Twariqa na Umoja, mshindi wa mchezo huo atakwenda kucheza fainali na Mikumi.
Mdhamini wa Mshindano ya Tambaza Ramadhani Cup Imran Baba, amesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kutoa elimu kuhusu maadili pamoja na kukuza vipaji vya vijana.
“Michezo ni muhimu katika maisha yetu ya kila siku, tuendee kuwa na upendo, nitaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya viwanja kwa kushirikiana na wadau mbalimbali” amesema Imran Baba.
Mratibu wa Mashindano ya Tambaza Ramadhani Cup Awadhi Dinongo, amesema kuwa mashindano yanaendelea vizuri, huku akibainisha kuwa mshindi wa kwanza anatarajia kupata Ng’ombe, jezi na kikombe, mshindi wa pili atapata Mbuzi na kikombe na mshindi wa watatu atapata jezi, mpira pamoja na kikombe.
“Tunamshukuru mdhamini wetu Imran Baba kwa ushirikiano wake mkubwa, pia tunaomba mashabiki waendelee kujitokeza katika mashindano Tambaza Ramadhani Cup ambapo fainali inatarajia kuchezwa tarehe 20/4/2023” amesema Dinongo.