Mwandishi Wetu
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bagomoyo imepokea vifaa mbalimbali vya uhifadhi taka ‘dustbin’ kutoka Fisher Record ya jijini Dar es Salaam.
Vifaa hivyo vimetolewa ili kuiwezesha wilaya ya Bagamoyo kukabiliana na uchafunzi wa mazingira unaotokana na taka ngumu.
Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Utawala na Uzalishaji kutoka Fisher Record, Motte Eliud amesema vifaa hivyo vitasambazwa Bagamoyo nzima na kila mwendo wa mita 100 kutakua na ‘ dustbin ‘.
“Kwa kuanzia tumeanzia hapa soko la samaki Dunda , lengo ni kusambaza kwenye wilaya zote za Tanzania Bara katika Mikoa yote 26.” Amesema
Nae, Majdi Mhina Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Bagamoyo akisoma taarifa ya Mkuu huyo wa Wilaya Halima Okash alisema Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ina jumla ya Kata 11 yenye vitongoji 167 na Ina wakazi 119,047 ambapo inazalisha taka ngumu tani 78 sawa na kg 0.66 kwa kila mkazi
Amesema, hali ya ukusanyaji na utupaji taka ngumu katika wilaya ya Bagamoyo inafanywa kwa kutumia Toyo za watu binafsi, gari moja ya halmashauri ambayo inasomba kwenye masoko, stendi na barabarani.
“Takwimu zinaonyesha wastani wa tani 25 sawa na asilimia 33 tu ya taka ndio zimekusanywa, kiasi cha taka kilichobaki kinasambaa kwenye maeneo mbalimbali kama vile kando kando ya barabara, kwenye maeneo ya wazi na kwenye Fukwe za Bahari.” Amesema Mhina
Pia, amesema hali ya ukusanyaji taka katika masoko, standi za mabasi, makazi, maeneo ya wazi ya barabara si za kuridhisha hii inatokana na kutokuwepo kwa ‘dustibin’ za kutosha hali hiyo inachangia mlipuko wa magonjwa kama vile Kipindupindu, Kuhara na Kuharibu Mifumo ya ikolojia.
“Kupatikana kwa vifaa hivi vitasaidia hali ya ukusanyaji wa taka katika maeneo yenye mkusanyiko ya watu wengi kama katika masoko, stendi,barabarani kutokana na kuwepo kwa vihifadhi taka na kurahisisha usimamizi wa usafi wa mazingira katika maeneo hapo.
Kwa upande wa Diwani wa kata ya Dunda Amir Mpwimbwi, amesema ujio wa vifaa hivyo utasaidia kutekeleza sheria ya mji mdogo ambapo mtua kitupa taka hovyo faini ni sh 50,000 au kifungo cha jela miezi sita au vyote kwa pamoja.