Na John Walter-Manyara
Kituo cha redio cha Smile Fm kilichopo Babati mkoani Manyara kimezindua rasmi kampeni ya KAMATA KITAA katika kata ya Magugu tarafa ya Mbugwe.
Kampeni hiyo yenye lengo la kutoa elimu kwa jamii kupinga vitendo vya Ukeketaji na Ukatili wa kijinsia mkoani Manyara imezinduliwa na mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii
Halmashauri ya wilaya ya Babati January Bikuba ambapo aliwataka wananchi kuripoti vitendo vya ukatili vinavyofanywa katika maeneo yao ili wahusika wachukuliwe hatua na hatimaye kumaliza vitendo hivyo katika jamii.
Amesema tabia ya kukaa kimya na kumalizana kimyakimya majumbani inachochea Ukatili kuendelea kushamiri kwa kuwa wahusika hawachukuliwi hatua huku wahanga wa vitendo hivyo wakiumia na kuathirika kisaikolojia.
Amesema jitihada na nguvu za Pamoja zinahitajika kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuweza kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia akiipongoza SMILE FM REDIO kwa kuanza kufanya kwa vitendo.
Amesema jitihada na nguvu za Pamoja zinahitajika kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuweza kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia akiipongoza SMILE FM REDIO kwa kuanza kufanya kwa vitendo.
Mkoa wa Manyara umetajwa kushika nafasi ya pili kwa matukio mengi ya ukatili wa Kijinsia huku ukishika namba moja kwa Ukeketaji watoto na wanawake.
Takwimu kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya Benki ya Dunia 2022, imeonyesha nchini Tanzania asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili lakini pia asilimia 17 wamefanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na pia alisema wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49 ambao ni asilimia 44 wameathiriwa na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Mwenyekiti wa SMAUJATA wilaya ya Babati Philipo Sanka na katibu msaidizi Rest Chuhila wamewasisitiza watoto kutokuogopa na badala yake waonapo vitendo vya ukatili au viashiria watoe taarifa kwa watu wanao waamini likiwemo dawati la jinsia na watoto polisi.
Kampeni ya kamata kitaa mwaka 2013 inakwenda sambamba na burudani mbalimbali pamoja na mchezo wa mpira wa miguu ambapo kwa mujibu wa Meneja wa Smile Fm redio Jeston Kihwelo washindi watakaopatikana watapatiwa zawadi na mdhamini mkuu katika kampuni ya Mati Super Brands Ltd kupitia kinywaji cha Tai.