Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza maadhimisho sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yafanyike katika ngazi ya mikoa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana Jumamosi (Aprili 15, 2023) wakati alipozindua Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)-Tunguu.
Waziri Mkuu Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameelekeza shughuli za maadhimisho hayo zifanyike kuanzia tarehe 17 Aprili, 2023 hadi siku ya kilele tarehe 26 Aprili, 2023.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa maadhimisho hayo ambayo yatafanyika kupitia Mikoa, Taasisi za Serikali na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama yaambatane na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, shughuli za kijamii hususan upandaji miti, usafi wa mazingira na mashindano ya michezo na sanaa mbalimbali.
Kadhalika, yaambatane na Mashindano ya uandishi wa Insha kwa shule za Msingi na Sekondari, mahojiano maalum na Wazee maarufu, midahalo na makongamano kuhusu Muungano na hatua ya maendeleo iliyofikiwa hadi sasa.
“Majengo yote ya Serikali yapambwe kwa vitambaa vyenye rangi sahihi za bendera ya Taifa, picha za Waasisi wa Muungano, Picha ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Tanzania Bara” Alisema Waziri Mkuu
Amesema kuwa Kwa upande wa Zanzibar majengo yapambwe kwa rangi sahihi za bendera ya Taifa, na picha za Waasisi wa Muungano na picha ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka huu ni “UMOJA NA MSHIKAMANO NDIYO NGUZO YA KUKUZA UCHUMI WETU”.