Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe. Joaquim Alberto Chissano ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kutunza na kuhifadhi kumbukumbu muhimu za historia ya harakati za Ukombozi wa nchi mbalimbali za Bara la Afrika ikiwemo Msumbiji.
Mhe. Chissano ameyasema hayo leo Aprili, 14,2023 jijini Dar es Salaam alipotembelea Kituo cha Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kilichopo eneo la Posta jijini Dar es salaam.
” Natoa pongezi kwa kazi kubwa uliyofanyika katika kituo hiki ya kuhifadhi na kuweka kumbukumbu ya kazi kubwa iliyofanyika tangu mwaka 1965, nafurahi kwamba kuna jambo kubwa limefanyika Tanzania” Amesisitiza Mhe. Chissano.
Amesema mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Bara la Afrika hautasahaulika kamwe kutokana na dhamira ya dhati ya Tanzania chini ya Uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa mstari wa mbele kushiriki katika ukombozi wa nchi nyingi za Afrika ikiwemo Msumbiji, Angola, Namibia,Zambia, Zimbabwe na Afrika ya Kusini.
Mhe.Chissano amebainisha kuwa Tanzania ilifanya maamuzi ya kuvipokea vyama na Wanaharakati wa ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika waliokua wakishindwa kuendesha siasa katika nchi zao kutokana na mazingira magumu kutawaliwa na ukoloni.
” Tanzania ilipopata Uhuru wake mwaka 1961 wapigania Uhuru wote na Vyama vya Ukombozi vilikuja Tanzania na Makao yao Makuu yalikua Tanzania” Amesisitiza.
Rais huyo Mstaafu wa Msumbiji amebainisha kuwa Baba Taifa Mwalimu k. Nyerere alikua ni kiongozi aliyefikika wakati wote akiongeza kuwa wao kama Chama cha FRELIMO walijifunzia Tanzania wakawa walimu wazuri.
Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, (Mb) akizungumza wakati wa mapokezi ya kiongozi huyo huyo ameeleza kuwa ziara yake katika Kituo cha Historia ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika inatoa historia kuhusu kuimarika kwa ushirikiano kati ya ya Tanzania na Msumbiji kupitia kazi kubwa iliyofanywa na Kamati ya Ukombozi wan chi za Afrika.
“Tumepata Faraja sana ya kutembelewa na wewe Mhe. Rais Mstaafu, Mzee wetu Joaquim Chissano, ninayo furaha kubwa kukukaribisha katika eneo hili, wewe ni mwenyeji hapa karibu sana nchini Tanzania. Msumbiji na Tanzania ni ndugu wa damu kutokana na historia iliyoasisiwa na waasisi wa Mataifa yetu mawili” Amesisitiza Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana.
Amempongeza Rais huyo Mstaafu wa Msumbiji kwa kuendelea kutumia Lugha ya Kiswahili akieleza kuwa Wizara yake inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuitangaza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Bara la Afrika kutokana na lugha hiyo kuwa silaha ya ukombozi.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji unaendelea kuimarika kutokana na uongozi shupavu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili vizazi vijavyo viendelee kunufaika.
Katika ziara hiyo viongozi mbalimbali wameshiriki wakiwemo Watumishi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndugu Saidi Yakubu, Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania,Wawakilishi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).