Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Bw. Abdallah Shaib Kaim akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Kituo cha Taarifa na Makumbusho ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Oswald Masebo
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Malikale, Bi. Rahel L. Kisusi, akisoma taarifa ya Miradi inayotekelezwa na Makumbusho ya Taifa Mkoani Lindi.
Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini Mhe. Hamida Mohamed Abdallah akiwa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mhe. Salima Kikwete katika shughuli ya uwekaji wa jiwe la Msingi katika Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Taarifa na Makumbusho ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika.
…………………..
Na Mwandishi Wetu, Lindi
Taasisi ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania imepongezwa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuimarisha uhifadhi wa malikale katika Mkoa wa Lindi.
Pongezi hizo zimetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Bw. Abdallah Shaib Kaim mjini Lindi wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Kituo cha Taarifa na Makumbusho ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika.
“Naipongeza Makumbusho ya Taifa la Tanzania kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kuhifadhi malikale katika mkoa wa Lindi. Hongereni sana’ amesema Bw. Kaim.
Bw. Kaim amewataka wananchi wa mkoa wa Lindi kushirikiana na Makumbusho ya Taifa katika kuhakikisha kuwa miundombinu mbalimbali iliyotengenezwa inatunzwa kwa uhifadhi endelevu.
Vile vile, kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kuwa ni chanzo muhimu cha upatikanaji wa maji duniani kote.
Aidha, wananchi wanaotokea jirani na eneo la mradi walijitokeza kwa wingi kushiriki katika kazi mbalimbali kituoni hapo.
Ushiriki huu ni muhimu kama Sera ya Malikale invyosema kuwa jamii ina haki ya kuelimishwa na kushirikishwa katika kutambua umuhimu wa malikale ya nchi kwa sababu nyingi ziko mikononi mwa jamii yenyewe.