Rais Mstaafu wa Msumbiji Mzee Joachim Chisano katika hafla ya tuzo ya utoaji wa tuzo ya Taifa Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu iliyofanyika kwenye Hoteli ya Rotana Posta Jijini Dar es Salaam Alhamisi Aprili 13,2023
Rais Mstaafu wa Msumbiji Mzee Joachim Chisano akimpongeza Zainab Ali Mabrouk kutoka Tanga mshindi wa tatu uandishi wa Riwaya inayoitwa “Nimelichungulia Kaburi” katika uandishi Bunifu kwenye hafla ya kwanza ya utoaji wa tuzo ya Taifa Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu iliyofanyika kwenye Hoteli ya Rotana Posta Jijini Dar es Salaam Alhamisi Aprili 13,2023. katikati ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda.
……………………………………………………….
Serikali na wadau mbalimbali nchini wametakiwa kuendelea kutambua mchango wa watu wanaoandika kwa kutumia lugha ya Kiswahili ili kulinda uhai wa lugha inayotumiwa kwa kiasi kikubwa Afrika Mashariki.
Akizumgumza katika Hafla ya ugawaji Tuzo ya Uandishi bunifu ya Taifa ya Mwalimu Nyerere, iliyofanyika katika Hoteli ya Rotana jijini Dar es Salaam, Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe. Joachimu Chissano, amesema kuwa ni muhimu kutambua juhudi na mchango wa wadau wa maandiko bunifu kwa lugha ya Kiswahili ili kuleta tija.
Mhe. Chissano aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesema kuwa ipo haja ya kuendeleza juhudi hizo ili kukuza uhai wa lugha ya Kiswahili kwani uwepo wa machapisho kunachangiwa kwa kiasi kubwa kukuza lugha.
“Natoa wito kwa Kamisheni kiswahili Afrika Mashariki, kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la nchi wanachama, kuendeleza matumizi ya Kiswahili katika maeneo muhimu ya kiutawala na kijamii kwani Kiswahili ni tunu na utambulisho wa Afrika na Mwafrika,” amesema Chissano.
Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo, Profesa Penina Mlama, amesema kuwa zoezi zima la kupokea miswada ya waandishi lilianza Septemba 12, 2023, na kukamilika rasmi Novemba 30, 2023.
Amesema kuwa Disemba 21, 2023, Tume ya Majaji ilianza kazi ya kuipitia miswada iliyokidhi vigezo vya kushindana, zoezi ambalo lilikamilika machi 30, 2023.
Amebainisha kuwa jumla ya miswada 283 ilipokelewa mbele ya kamati, miswada 193 ikiwa ni ya ushairi, 85 ya riwaya na miswada mitano ya kazi ambazo zilikuwa hazishindanishwi.
Ameeleza kuwa kati ya miswada hiyo, 79 haikukidhi vigezo vya kushindana, huku 204 ndiyo iliyokidhi vigezo vya kushindana ili kumpata mshindi, pia ujumla, miswada 254 ilitokea Tanzania Bara na miswada 29 ilitokea Zanzibar, huku idadi ya wanaume walioshiriki ni 223 na wanawake 60.
“Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza waandishi bunifu wote walioshiriki katika kushindania tuzo hizi, hata kama hutabahatika kuwa mshindi, ukumbuke kwa kuthubutu kwako kukaa na kubuni ushairi, au riwaya, umeupaisha uandishi bunifu wa Kiswahili nchini kwetu kwenda kwenye kiwango kingine,” amesema Profesa Mlama.
Profesa Mlama ametoa wito kwa waandishi bunifu kujiandaa kwa msimu unaokuja wa mwaka 2024, ambao utatangazwa rasmi hapo Juni 1, 2023, ambao dirisha la kupokea miswada litafunguliwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Profesa Kitila Mkumbo, amesema kuwa ni muhimu kwa nchi kuwa na watu wanaoandika kwani maandishi ni moja wapo kati ya nyenzo ya vita ya utamaduni.
“Nchi nyingi ziko makini na watoto wao wanasoma nini ?, hata nchi ambazo zinajifanya zina demokrasia sana, wewe huwezi kutoka tu hapa, ukaenda Marekani, ukaweka kitabu chako maktaba, hicho kitu hakipo. Lazima wajue watoto wao wanasoma nini.” amesema Profesa Mkumbo.
Jumla ya washindi 20 walitangazwa katika hafla hiyo, 10 wakiwa washindi wa riwaya na 10 wakiwa wa ushairi , washindi saba kutoka kila tanzu walipewa vyeti vya kuwatambua, huku watatu, kutoka kila tanzu wakipewa vyeti na fedha taslimu.
Mshindi wa tatu kutoka kila tanzu amepewa zawadi ya Shilingi milioni tano; mshindi wa pili Shilingi milioni saba, huku mshindi wa kwanza akijizolea Shilingi milioni kumi.
Washindi hao ni Amri Rajab Abdalah, mwandishi bunifu kutoka Kilimanjaro, ambaye ameibuka mshindi kwa upande wa tanzu ya ushairi, huku akiupa mswada wake huo jina la Mtale wa Ngariba.
Hamis Hussein Kibari, kutoka Dar es Salaam, ameibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa riwaya.
Tuzo hizo zilizinduliwa rasmi Septemba 12, 2022, ambapo imeandaliwa kama sehemu ya juhudi za Serikali kuunga mkono uandishi wa kazi bunifu, tasnia ya uchapishaji, pamoja na kukuza utamaduni wa kujisomea miongoni mwa Watanzania.
Ikipewa jina la Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, kama sehemu ya kuenzi mchango wa mwanasiasa na mwanafalsafa huyo katika eneo la uandishi wa kazi bunifu, tuzo hiyo imetolewa Aprili 13 ili kuendana na sherehe ya kuzaliwa kwa kiongozi huyo anayeheshimika ndani na nje ya nchi.