Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa kituo cha polisi Orkesumet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Mrakibu wa polisi (SP) Christina Mkonongo ametoa elimu ya polisi jamii kwa mashabiki na wachezaji katika fainali ya mashindano ya Polisi Jamii Cup 2023 Simanjiro yaliyofanyika katika viwanja vya Tanzanite Complex Stadium (kwa Mnyalu) Mji mdogo wa Mirerani.
SP Mkonongo ametoa elimu ya polisi jamii kwa mashabiki pamoja na wachezaji kuhusiana na mada wakati wa mapumziko ya fainali hiyo ambapo timu ya Polisi SC iliifunga Tanesco SC kwa mabao 4-3.
Akizungumza kwenye michuano hiyo amesema jamii inapaswa kuzingatia utii wa sheria bila shuruti na kutojichukulia sheria mkononi.
“Jamii inapaswa kutojihusisha na uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya na kutojihusisha na masuala ya ushoga na mapenzi ya jinsia moja,” amesema SP Mkonongo.
Amesema utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa polisi kata ili zifanyiwe kazi, ulinzi jirani na ulinzi shirikishi, ukatili wa kijinsia na madhara yake katika jamii.
“Pia hivi sasa kuna mmomonyo mkubwa wa maadili kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini, hivyo jamii inatakiwa kuhakikisha watoto wadogo wanapata malezi na makuzi mema kwa wazazi na walezi ili kuandaa raia wema wa miaka ijayo,” amesema SP Mkonongo.
Mkuu wa polisi Wilaya ya Simanjiro, Mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP), Mathayo Mmari akizungumza kwenye michuano hiyo, amesema mashindano hayo yana lengo la kupinga vitendo vya ukatili, mmomonyoko wa maadili na matukio mengine ya uhalifu wilayani humo.
SSP Mmari amesema kwa kupitia falsafa ya polisi Jamii na ulinzi shirikishi itasaidia kuiweka jamii karibu na polisi, jambo litakalowezesha kupata taarifa za uhalifu kwa urahisi na kuwaondoa wananchi hofu iliyojengeka kwa polisi.
Amesema wameandaa mashindano hayo ikiwa ni utaratibu uliopo chini ya IGP Camillus Wambura lengo likiwa kutoa elimu juu ya tabia hatarishi na vijana kuwa na afya bora kupitia michezo hivyo kuwaepusha vijana kuacha tabia za matumizi ya dawa za kulevya, bangi na ulevi ambavyo huchangia kuzorotesha uchumi wa nchi.
Mwenyekiti wa chama cha soka wilaya ya Simanjiro (SIDFA), Charles Mnyalu amewapongeza polisi kwa kuanzisha michuano hiyo ambayo itachangia vijana kushiriki michezo.