Serikali imesema inaendelea kuyatumia majina yaliyotolewa katika kipindi cha utawala wa kikoloni kulinda uhifadhi wa historia na rasilimali zilizopo nchini kwa manufaa ya Taifa na kwamba kwa sasa hakuna umuhimu wa kuyabadili majina hayo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Sophia Mwakagenda aliyetaka kujua lini Serikali itabadili majina ya Kigeni kuwa ya Kitanzania kwenye Rasilimali za Taifa akitolea mfano wa Mlima Livingtone na Ziwa Victoria.
Mhe. Masanja ameongeza kuwa Serikali inatumia majina ya Kigeni katika baadhi ya Rasilimali za Taifa kwa lengo la kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa na kwamba majina hayo yaliyotolewa kipindi cha utawala wa ukoloni na maeneo hayo yameendelea kufahamika kihistoria kutokana na kutangazwa na kuandikwa kwenye nyaraka na vitabu mbalimbali.
“Serikali haioni haja ya kubadili majina ya maeneo hayo ambayo kwa sasa yana mchango mkubwa kiuchumi kwa Taifa letu kwani tunaitangazia dunia na kuonyesha jinsi tulivyojaaliwa na rasilimali za msingi” Mhe. Masanja amesisitiza.
Aidha, ameweka bayana kuwa Serikali itaendelea kuzingatia majina ya wazawa kwenye rasilimali mbalimbali za Taifa kadri zinavyoanzishwa.