…………………
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga Aprili 12, 2023
katika Stendi ya Mabasi Kabwe Jijini Mbeya, amezindua wiki ya nenda kwa
usalama barabarani Kimkoa kwa kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto,
magari, pikipiki na bajaji pamoja na kubandika Stika za nenda kwa usalama
barabarani.
Akizindua wiki ya nenda kwa usalama barabarani kimkoa, Kamanda Kuzaga
amewataka madereva wa Pikipiki, Bajaji, Magari madogo na magari ya abiria
kuhakikisha vyombo vyao vya moto zinakaguliwa na wakaguzi wa magari wa
Jeshi la Polisi waliopo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ili
kuangalia ubora wake na kama vina sifa ya kutembea barabarani.
Aidha, ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na
Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya na wakuu wa vyuo vya udereva
mkoa wa Mbeya wameandaa mafunzo maalum ya wiki moja kwa madereva
wenye leseni lakini hawakupita katika vyuo vya udereva pamoja na wale ambao
hawana leseni ili waweze kujifunza na hatimaye kupata cheti cha udereva
kutoka katika chuo kinachotambulika na serikali.
Naye, Mwenyekiti wa Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Eng. Rajab Ghulika
amewataka madereva kujitokeza kuhudhuria mafunzo ya udereva ili kuwajengea
uwezo na umahiri wa matumizi ya vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na
kujikumbusha alama na michoro mbalimbali ya usalama barabarani.
Wiki ya nenda kwa usalama barabarani imeambatana na ukaguzi wa vyombo
vya moto, ubandikaji stika za nenda kwa usalama, utoaji wa elimu ya usalama
barabarani kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara Pamoja na utoaji
wa mafunzo maalum ya udereva kwa madereva na utoaji vyeti vya udereva kwa
wahitimu. Kilele cha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani
kitafanyika Aprili 20, 2023 katika uwanja wa Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya.
Imetolewa na:
BENJAMIN E. KUZAGA – ACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.