Mchungaji wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT) Parishi ya Sabasaba Singida, Yona Ezekiel akitoa baraka kwa waumini wa kanisa hilo (hawapo pichani) wakati wa Ibada ya Pasaka iliyofanyika Aprili 9, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KANISA la Moravian Tanzania Parishi ya Sabasaba mkoani Singida limeiomba
Serikali kuzifuta Taasisi zote zisizo za Kiserikali (NG’OS) ambazo zinatuhumiwa
kuhusika kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja (shoga)
Ombi hilo limetolewa na Mchungaji wa kanisa hilo, Yona Ezekiel wakati
akihubiri jana katika ibada ya Pasaka ambapo alisema Serikali ichukue hatua za
haraka kuyafuta mashirika hayo kwani watanzania hawavitaki vitendo hivyo.
Alisema hivi karibuni aliyekuwa Mbunge wa Kyela na kushika nafasi
mbalimbali za uwaziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.
Harison Mwakyembe alisema zipo taasisi nyingi ambazo zimeenea hadi mikoani
ambazo zinahamasisha ushoga na wakurugenzi wa taasisi hizo wanajulikana na kuwa
walengwa ni vijana.
“Tumeambiwa na Dk. Mwakyembe kuwa taasisi hizi zipo na wahusika nazo
wapo tunaiomba Serikali izifute kwani zina waharibu vijana ambao ni nguvu kazi
ya taifa na watanzania awahutaki ushoga, usagaji na ukatili wa kijinsia wa aina yoyote kwani na hata vitabu vya dini vimekataza mambo hayo,” alisema Mchungaji Yona.
Akihubiri huku akilia na kulifanya kanisa lote kulipuka kwa vilio Mchungaji
Ezekiel alisema nchi yetu isikubali kuingia katika vitendo hivyo kwa shinikizo
la kupata fedha za mikopo kutoka kwa matajiri ambapo aliwaomba wazazi kuendelea
kufuatilia nyendo za watoto wao ambao ndio wa lengwa wa mambo hayo.
Akizungumzia kufufuka kwa Yesu Kristo baada ya kifo chake huku akinukuu
kitabu cha Yohana Mtakatifu Sura ya 20 mstari wa kwanza hadi wa nane alisema
kufufuka kwake ni ushindi mkubwa kwani Mungu alimleta duniani ili kuja kuwakomboa wanadamu kutokana na
dhambi.
Alisema kifo wakati wote kimekuwa kikiharibu mipango ya watu, kinaleta
majonzi, huzuni,mtetemeko na kuwa
hakivumiliki kwani hakichagui mtu na kimekuwa kikiwachukua hata watu waliokuwa
wakitegemewa na ndugu na familia zao na ndivyo ilivyokuwa kwa Yesu ambaye kifo chake
kilikuwa na fumbo kubwa la imani kwani aliuawa na siku ya tatu alifufuka.
Mchungaji Ezekiel alitumia ibada hiyo ya Pasaka kuwahimiza wakristo kuacha
kutenda dhambi na badala yake kuwa na moyo wa huruma wa kusaidia watu mbalimbali wenye
uhitaji wakiwepo Yatima, Wajane, wazee, wagonjwa, wafungwa na wengine wote na
kuwa kwa kufanya hivyo watabarikiwa na Mungu.