Katibu MKuu Wizara ya Maliasili na utaliii, Dk.Hassan Abbas amewataka wahifadhi wasiokuwa tayari kutekeleza misingi ya pamoja waliyojiwekea katika kuhakikisha misitu inahifadhiwa nchini kutafuta mahala pengine pa kazi huku akieleza kuwa nyakati tamu na chungu zinakuja.
Akizungumza leo Aprili 8, 2023 wakati alipokutana na menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS kujadili, kuchakata na kupeana miongozo inayolenga kupeleka mbele majukumu ya uhifadhi waliyonayo, Dk. Abbas amesema
anatambua umuhimu wa sekta ya misitu nchini na hayuko tayari kuona mtu yoyote anakwamisha uhifadhi nchini.
“Sekta hii ya misitu pamoja na kujishughulisha na mambo mengine kwenye misitu ni sekta ya kiuchumi, ni muhimu sana kwa uchumi wa taifa letu, inaingiza mabilioni ya fedha katika Serikali lakini pia kwenye uchumi wa nchi kwa ujumla wake, lakini leo nataka niwaambie mnatumikia sekta ya kiroho! Misitu ndio chanzo cha uhai,”
“Misitu ni sehemu ya uhai wa mwanadamu, tukicheza, tukashindwa kuwa na misimamo, tukafanya mambo ya ajabu misitu ikatoweka maana yake Bustani ya Edeni imetoweka kwenye uso wa dunia, kwa hiyo leo nimepita kuwaambia kuwa tunawaona, tunawaangalia na kuwatazama.” anasema Katibu Mkuu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu alisema hatafafanua kauli ya kuwaona, kuwaangalia na kuwatazama hadi wakati mwingine huku akiitaka menejimenti ya TFS kufikisha ujumbe kwa askari, maafisa na wafanyakazi wengine walio na mikataba na wale wasiopo kwenye kundi lolote lakini ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya TFS watambue Wizara na Serikali inatambua na kuthamini kazi wanayoifanya.
Akifafanua zaidi Katibu Mkuu Dk. Abbas amesema kuwa, anaposema Serikali inawathamini wahifadhi inamaana kwamba katika kila wanachokifanya itakuwa pamoja nao, pakuwatetea itawatetea, pakuwafanya waeleweke itapambana waeleweke, “hatutakuwa aina ya viongozi wa hiyo mimi sikujua, kwa kweli hio mimi ndio nasikia, tutasema hili tuliamua, kama kunguka tuanguke, kama kupanda tupande nalo, sisi ndio aina ya viongozi mliowapata kwa sasa.”
Aliongeza kuwa uongozi mpya wa Wizara ya Waziri wa Maliasili na Utalii umekusudia kubadilisha mifumo yote ya utendaji wa kimazoea ili kuhakikisha kile kinachokusudiwa na viongozi wao kinatekelezwa. Hivyo kama kuna wahifadhi wenye tabia ya kuzembea, husuda, chuki, vizabizabina, wenye uchu wa madaraka, wasiotoa ushirikiano ili wengine washindwe kutimiza wajibu wao watawapa muda wa kubadilika na iwapo watashindwa waondoke ili nafasi walizopewa wapewe wengine wenye uwezo wa kuzifanya kwa uadilifu na uaminifu kwani nyakati chungu na tamu zinakuja. Aidha ametumia nafasi hiyo kuwataka watendaji wote kuacha kukaa ofisini na badala yake waende kusikiliza na kutatua changamoto zilizopo pamoja na kujenga uhusiano baina ya Wakala huo na wadau. “Kazi kubwa ya uhifadhi mnafanya lakini kama hamuwasiliana na wadau wenu ili wawaelewe, kuwaamini na kuwakubali ni kazi bure, imarisheni mawasiliano ya ndani na nje.” Pia Katibu Mkuu Dk. Abbas alitoa somo la siri nane za mafanikio ambazo ambazo ni kuwa na malengo yanayoeleweka, kujiwekea malengo makubwa (Olympic goals), kusimamia utekelezaji, kuzingatia muda, ushirikiano, mawasiliano, maadili na kumpa Mungu nafasi katika kila jambo ambapo aliitaka menejimenti pamoja na wahifadhi wote TFS kutumia kama muongozo wao katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, ameeleza mipango mbalimbali waliyonayo katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao huku akiushukuru uongozi wa Wizara kwa kutoa maelekezo na miongozo mbalimbali inayolenga kuboresha utendaji wao.
Hii ni mara ya pili kwa Katibu Mkuu Dk. Abbas kukutana na menejimenti ya TFS tangu kuteuliwa kwake kwa lengo la kutoa muongozo na kusisitiza yaliyosemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa wiki chache zilizopita walipotembelea kwa pamoja Wakala huo. Tulizo Kilaga anaripoti.