Na WMJJWM, DAR ES SALAAM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima amewaomba wanamichezo kupitia Vilabu vyao kuungana na Serikali kupaza sauti ya kuhamasisha wananchi kudhibiti mmomonyoko wa maadili unaochochea vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwa watoto.
Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito huo alipokutana na rais wa Klabu ya Yanga Mhandisi Hersi Said Aprili 7, 2023 jijini Dar es salaam ikiwa na mwanzo wa ziara yake ya kutembelea vilabu vya Michezo kuhamasisha wanamichezo kushiriki kampeni ya ZIFIUKUKI(Zijue Fursa, Imarisha Uchumi, Kataa Ukatili, Kazi Iendelee)
Akiilezea kampeni hiyo Dkt. Gwajima amesema lengo lake ni kuelimisha jamii kuhusu fursa mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi eneo ambalo wananchi wengi wanaonekana kutofahamu hasa wa viijijini na wengine wa mijini lakini mifumo ya taarifa haiwafikii.
Waziri Dkt. Gwajima amesema Ajenda ya kulinda maadili ya jamii ni Jambo la kitaifa hivyo ni muhimu sekta zote hususani Michezo ambako kuna wafuasi wengi, ikiwemo ya Klabu za Mipira, Michezo na Sanaa mbalimbali kupitia majukwaa yao pamoja na mitandao ya kijamii kulisemea.
Ameongeza kwamba, Wizara inaimarisha ushirikiano na jamii ili ajenda hizi zimilikiwe na Jamii yenyewe.
Tamasha la ZIFIUKUKI ni muendelezo wa Kampeni ya Wizara ya Twende Pamoja Ukatili Tanzania sasa Basi iliyozinduliwa mwaka 2018 kwa sura ya Matamasha ya kuelimisha Jamii kuhusu fursa za Kiuchumi sambamba na kuhamasisha jamii kudhibiti mmomonyoko wa maadili na kupinga ukatili wa kijinsia na kwa watoto.
Tamasha hilo litakalotembea mikoa yote litazinduliwa 27 Aprili 2023 Viwanja vya Leaders Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mhandisi Hersi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuona umuhimu wa kushirikisha Klabu za Michezo na kwamba, ajenda hiyo ni muhimu na Klabu ya Soka ya Yanga ipo tayari kutoa ushirikiano wote kuhakikisha maadili ya jamii ya kitanzania yanaimarika na wananchi wote wanatambua fursa za kiuchumi na kunufaika ili kuunga mkono juhudi za Serikali.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Manara TV ambayo ina ushirikiano wa karibu na Klabu ya Soka ya Yanga imeunga mkono ajenda hii na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufikisha ujumbe kwa Jamii na kuhamasisha kuchukua hatua sahihi kwa Maendeleo na Ustawi wa jamii.