………………….
Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dodoma
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa mradi wa uwanja wa kupumzikia wananchi lililopo eneo la Nanenane kata ya Nzuguni jijini Dodoma.
Dkt. Chana amesema hayo Aprili 6, 2023 jijini Dodoma wakati akikagua shughuli za ujenzi uwanja huo ambao unajengwa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) na kusimamiwa na Mshauri Mwelekezi ambaye ni Chuo Kikuu Ardhi kilichopo jijini Dar es Salaam.
“Tumekuja kuangalia uwanja huu wa michezo ambao unajengwa hapa Dodoma, tunatambua kwamba Dodoma ni makao yetu makuu, tunahitaji miundombinu ya kutosha. Sisi kama Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tupo hapa kuona kazi hiiinaendelea na tumewaelekeza wakandarasi lazima wafanye kazi hii kwa muda ambao tumekubaliana” amesema Dkt. Chana.
Ujenzi wa mradi huo una awamu tatu za utekelezaji wa ujenzi wa eneo changamani la michezo Dodoma, awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa eneo la kupumzikia wananchi ambalo ni sehemu ya Uwanja wa Michezo Dodoma linajumuisha jingo la utawala, viwanja viwili vya mpira wa miguu, hostel watakapokuwa wanafikia wanamichezo, vyoo na chumba cha wanamichezo kubadilishia nguo wanazotumia wkati wa michezo.
Aidha, Dkt. Chana amesema wizara hiyo imedhamiria kuwa kila mkoa na wilaya zinakuwa na viwanja vya michezo yenye kukidhi hadhi za kimataifa ambao watu watakuwa wanakutana na kufurahia masuala ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Michezo inaongeza muda wa kuishi, inapunguza magonjwa watanzania tutakuwa imara na ukiwa imara unachapa kazi na kuwa na maisha ya furaha na Amani, siyo lazima mpaka Daktari akuambie nenda kafanye mazoezi. Michezo ni sehemu ya maisha yetu, mazoezi ni sehemu ya maisha yetu” Dkt. Chana.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo Mshauri Mwelekezi ambaye pia ni Msanifu Mjengo Bw. Nayingo Peter kutoka Chuo Kikuu Ardhi amesema kuwa wakiwa kama mshauri mwelekezi eneo changamani la michezo Dodoma lina ukubwa wa ekari 328 litahusisha pia ujenzi wa eneo la kupuzika wananchi ambalo litagharimu takriban bilioni 13 ambalo linatarajiwa kukamilika kwa muda wa miezi 12 sawa na mwaka mmoja huku awamu zote tatu zikitarajiwa kukamilika kwa takriban miezi 32 sawa miaka miwili na miezi nane.