Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson akizungumza bungeni kuhusu watumishi wa serikali wanaojitolea kupewa kipaumbele Cha ajira.
…………………………….
NA WAF- BUNGENI DODOMA.
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Akson ameitaka Wizara ya Afya na OR TAMISEMI kukaa pamoja na OR Utumishi na Utawala bora kuja na mfumo utaowatambua Watumishi wanaojitolea katika maeneo ya kutolea huduma ili wapewe kipaumbele pindi nafasi za ajira zitakapotolewa.
Dkt. Tulia amebainisha hayo leo Jijini Dodoma katika Mkutano wa 11 kikao cha tatu, wakati Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akitoa majibu kwa Mbunge wa viti maalumu Mhe. Felister Deogratius Njau juu ya ajira kwa Watumishi wanaojitolea katika vituo vya kutolea huduma.
“Mhe. Waziri wa afya na Waziri wa TAMISEMI nafikiri kuna haja ya kukaa na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Watumishi wa afya wanaojitolea na walimu wanaojitolea huwa haipendezi sana, yani kwamba wao ndio hawana sifa za ajira au”. Amesema Dkt. Tulia
“Nafikiri utengenezwe utaratibu mzuri ili kila mwaka kuwe na taarifa za wanaojitolea ili ajira zinapopatikana zitumie taarifa hizo kwenye mfumo kuwapa wao kipaumbele.” Ameendelea kusisitiza Dkt. Tulia.
Akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Wizara ya Afya imetoa mwongozo wa kuwalipa nusu mshahara kwa mapato ya ndani Watumishi wanaojitolea, huku akisisitiza hospitali za Mikoa, Kanda na Taifa zimeweza kuwalipa hadi 40% ya Watumishi wote wanaojitolea mshahara kamili kwa mapato ya ndani.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Wizara itashirikiana na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora ili kuona namna bora ya kuwapa kipaumbele Watumishi ambao wamekuwa wakijitolea kwenye vituo vya kutolea huduma kuliko waliopo nje wakisubiri ajira.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema Wizara itaendelea kupeleka Watumishi katika maeneo mbalimbali kwa kuangalia mzigo wa wagonjwa waliopo katika eneo hilo ili wananchi wapate huduma bora.