Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bi. Esther Mkokota akizungumza katika mkutano wa ‘TAKUKURU Rafiki’ leo tarehe 5/4/2023 katika Kata ya Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Wenyeviti Kata ya Chamazi Bw. Bernard Haule kizungumza katika mkutano wa ‘TAKUKURU Rafiki’ leo tarehe 5/4/2023 katika Kata ya Chamazi jijini Dar es Salaam.
Wananchi wa Kata ya Chamazi jijini Dar es Salaam wakiwa katika mkutano wa ‘TAKUKURU Rafiki’ kwa ajili ya kutoa kero kutokana na watoa huduma kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo sekta ya maji, elimu, afya nishati kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.
……………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wananchi wametakiwa kuwa mstali wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya rushwa pamoja na kuhoji kwa viongozi au wasimamizi pale wanapoona mradi umeshindwa kumalizika kwa wakati tofauti na makubaliano.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Chamazi leo tarehe 5/4/2023 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa ‘TAKUKURU – Rafiki’ Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bi. Esther Mkokota, amesema kuwa lengo la programu ya ‘TAKUKURU – Rafiki’ ni Kuzuia vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma za kijamii pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea.
Amesema kuwa ni fursa kwa wananchi kutaja kero wanazozijua kupitia idara mbalimbali ikiwemo maji, elimu, nishati, afya ili ziweze kufanyiwa kazi na kutafutiwa ufumbuzi kwa wakati.
“Tunakwenda kuzitaja hizo kero lengo ni kwenda kuzitafutia ufumbuzi, sisi kama wananchi tuna haki ya kujua miradi inayotekelezwa ili ujue inachukua muda gani kumalizika jambo ambalo litakusaida kuhoji pale utakapoona inakwenda kinyume na makubaliano katika utekelezaji wake” amesema Bi. Mkokota.
Amesema kuwa wapo viongozi na wananchi wasiokuwa wahadilifu kwani wamekuwa wakifanya vitendo ambavyo sio rafiki katika utekelezaji wa miradi.
Bi. Mkokota amesema kuwa kero za wananchi zikiachwa pasipo kutatuliwa au kupatiwa ufumbuzi zinaweza kusababisha kutokea kwa vitendo vya rushwa katika jamii na kuleta usumbufu mkubwa.
Amebainisha kuwa programu ya ‘TAKUKURU – Rafiki’ inachangia kukuza ustawi wa utawala bora kwa kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika utoaji wa huduma kwa umma au katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Programu hii itasaidia kuongeza uzingatiaji wa misingi ya utawala bora, ushirikiano wa kila mwananchi na wadau katika kupambana dhidi ya rushwa na kuaminika kwa serikali kwa jamii inaowahudumia” amesema Bi. Bi. Mkokota.
Akizungumza kwa niaba ya Diwani wa Kata ya Chamazi, Mwenyekiti wa Wenyeviti Kata ya Chamazi Bw. Bernard Haule, amesema kuwa amefurai ujio wa ‘TAKUKURU Rafiki’ kwani umeleta hoja ya kuzuia rushwa.
Amesema kuwa wananchi wa Kata ya Chamazi watakwenda kuifanyia kazi ya elimu ya ‘Takukuru Rafiki’ kwa sababu Kuzuia rushwa ni jukumu la kila mtu.
“Natamani elimu hii iendelee mara kwa mara katika kata ya Chamazi kwa sababu elimu hii inakwenda kuondoa mabango wakati Mhe. Rais anapopita, lakini kupitia programu hii TAKUKURU inafanya kazi” amesema Bw. Haule.
Wakizungumza katika Mkutano wa ‘TAKUKURU Rafiki’ wakazi wa Kata ya Chamazi, Manispaa ya Temeke wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke kufatilia utekelezaji miradi mbalimbali katika sekta ya maji, elimu, afya, nishati, ardhi kutokana baadhi ya huduma hizo zinatolewa kwa kujuana jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
Mkazi wa Kata ya Chamazi Omary Juma amesema kuna ukosefu wa huduma ya umeme katika eneo la kiponza pamoja na Buyuni jambo ambalo linaleta usumbufu na kero kubwa, huku akibainisha kuwa wamefatilia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) bila mafanikio.
“Kuna urasimu katika usambazaji wa huduma ya umeme, unalipia huduma siku moja na mwenzako, lakini yeye anawai kuwekewa, huku mwengine wanamcheleweshewa bila sababu ya msingi” amesema Bw. Juma.
Ameeleza kuwa pia wana shida ya huduma ya maji, kwani awali waliambiwa na DAWASA kuna mradi ambao utakuwa msaada kwao, lakini mpaka sasa hakuna mafanikio yoyote, hivyo wameiomba Takukuru wawasaidie kufatilia ili kujua ukweli wapi umekwama.
Bw. Idrisa Mahiyadi amesema kuwa katika Shule ya Sekondari ya Mbande wazazi wanachangishwa michango mingi bila sababu, huku Shule Kisewe kuna ukosefu wa madarasa ukilinganisha na idadi ya wanafunzi katika shule hiyo.
“Walimu wanadai pesa kusaisha mithiani, kuna michango ya rambi rambi kila wakati, pia shule ya kiponza inachelewa kujengwa” amesema Bw. Mahiyadi.
Hata hivyo wamebainisha kuwa ili kuondokana baadhi ya changamoto ikiwemo mchango wa rambi rambi kila mkondo unapaswa kuchangia tatizo husika badala ya tatizo la mwanafunzi mmoja kwa shule nzima.