Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa Maji Orkesument ulioimarisha hali ya upatikanaji wa Huduma ya maji safi kwa wananchi na mifugo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa maji unaotajwa kugharimu zaidi ya Bilioni 41.5 katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Aidha Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira chini ya uongozi wa mwenyekiti wake Jackson Kiswaga imefika kujionea maendeleo ya mradi huo ambao Kwa asilimia kubwa umekuwa chachu ya maendeleo Kwa jamii ya wafugaji Katika maeneo hayo.
Pia, Kamati hiyo imeagiza kuendelea kufanywa maboresho ikiwemo kuongeza maeneo ya kunyweshea maji mifugo (mbauti) Ulinzi wa vyanzo vya maji pamoja na utunzaji wa miundombinu hiyo ya mradi.
Kwa upande wake Waziri Mwenye dhamana ya maji Mh Aweso amesisitiza kuwa kazi iliofanyika Simanjiro imefanyika maeneo mengine mengi nchini na kueleza kuwa Wizara ya Maji inaendelea na kazi maeneo yote yenye changamoto ya Maji nchini.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso ameelekeza kutolewa Milioni 500 Kwa ajili ya maboresho ya Huduma Kwa baadhi ya Vijiji zaidi ya Nane (8) ili Vijiji hivyo viendelee kupata Huduma ya maji Kwa ukaribu zaidi.
Kwa upande wao baadhi viongozi na wananchi wa maeneo hayo wameendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan Kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi kwa maslahi ya Wananchi wa vijijini ikiwemo wakazi wa eneo la Mji mdogo la Orkesument Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.