Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam, imekabidhi madawati 300 yenye thamani ya shilingi milioni 38 kwa shule ya msingi Kunduchi jijini Dar es Salaam na kufikisha idiadi ya madawati zaidi ya 2,300 yenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 300 ambayo yameshatolewa na klabu hiyo kwa shule mbalimbali hapa nchini.
Madawati hayo yalipokelewa na mkuu wa wilaya ya Kindondoni Saad Mtambule katika shule hiyo iliyopo kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Kupokelewa kwa madawati hayo 300 kunaifanya shule ya msingi Kunduchi kuondokana kabisa na tatizo la uhaba wa madawati shuleni hapo na hivyo kuanzia sasa wanafunzi wte wa shule hiyo watakuwa wanakaa kwenye madawati kwani kabla ya msaada huo, shule hiyo ilikuwa na uhaba wa madawati 300.
Rais wa klabu ya Rotary ya Dar es Salaam Nikki Aggarwal, amesema klabu hiyo imekuwa ikishirikiana na jamii ili kuboresha huduma za jamii na mradi wao mkubwa wa jamii ni kusaidia katika sekta ya elimu kwa kuchangia madawati.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni ameishukuru klabu hiyo na kuiomba kuendelea kuchangia kwatika kuimarisha sekta ya Elimu katika wilaya hiyo.
Amesema wilaya ya Kinondoni imekuwa kinara katika kufaulisha wanafunzi na kwamba mafanikio hayo yasingeweza kutokea bila jitihada za dhati za serikali na wadau kama rotary kuwekeza katika elimu.