Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar . 02-04-2023.
Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Mheshimiwa, Dkt.Khalid Salum Mohamed amesema katika kuwaenzi viongozi wa kitaifa ipo haja ya kuandikwa historia zao ili vizazi viweze kupata kumbukumbu sahihi za viongozi hao.
Hayo ameyasema huko Kiembe Samaki, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja wakati wa kufanya ziara na kusoma dua katika kaburi la Kamishna Msaidizi Muandamizi wa Jeshi la Polisi Marehemu Khamis Darwesh Mdingo na Kaburi la Kanal Mstaafu Marehemu Seif Bakari Omar .
Amesema kila nchi ina utaratibu wake wa kuwaenzi viongozi wake kutokana na sababu zake, kwani wao ndio chimbuko la Mapinduzi ya mwaka 1964 ambayo yalileta uhuru, usawa pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi ambayo matunda yake yanaonekana hadi sasa .
Aidha alisema kuwa viongozi hao wa kitaifa walifanya mengi katika nchi hii kutokana na jasho lao ikiwemo kuunganisha Nchi mbili kati ya Tanganyika na Zanzibar na kupata muungano wa Tanzania .
Alifahamisha kuwa Serikali imeandaa utaratibu wa kisheria wa kuwaenzi viongozi wa kitaifa katika sheria ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2021 iliyoweka utaratibu ya wiki wa kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa na Waasisi wa Mapinduzi
Nae Msemaji wa Familia Jafar Abdalla Mussa akitoa neno la shukrani kwa niaba ya familia hiyo kwa kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ujio huo wa kufanya ziara ya kusoma dua kwa Marehemu wazee wao .
Aidha ameiyomba Serikali kuwa karibu na vizazi vya marehemu hao ili kupata msaada mbali mbali unapohitajika katika familia hiyo .
Ibada ya kuwaombea dua Marehemu Khamis Darwesh Mdingo na Marehemu Seif Bakar Omar imeongozwa na Kadhi wa Wilaya Sheikh Hemed Saleh Ali .
Maadhimisho ya Wiki ya Kuwaezi Viongozi wa Kitaifa, Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Katibu wa Kwanza wa Chama cha Afro Shirazi na Siku ya Kumbukumbu ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume hufanyika kila mwaka katika wiki ya mwanzo wa mwezi wa nne