Naibu Katibu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Switbert Mkama (katikati) akishuhudia makabidhiano ya funguo ya pikipiki mbili kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Hamad Mapengo (kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai Wilayani humo.
Naibu Katibu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Switbert Mkama (katikati) akishuhudia makabidhiano ya funguo ya pikipiki mbili kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Hamad Mapengo (kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai Wilayani humo.
Moja kati ya pikipiki saba zilizonunuliwa na Serikali kupitia Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai. Pikipiki hizo zenye thamani ya TZS 36.2 Milioni zimekabidhiwa katika Halmashauri za Wilaya ya Tanganyika, Mpimbwe, Iringa, Mbeya, Mbarali, Wanging;ombe na Sumbawanga.
5. Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Switbert Mkama akipanda mti katika kijiji cha Ntibili, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai. Ziara hiyo.
…………….,…………..
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema haitavumilia ubadhilifu wa aina yoyote katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini na badala yake itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha thamani ya fedha inaendana na miradi itakayotekelezwa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai Tanzania aliyoifanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Dkt. Mkama amesema Serikali ya Awamu Sita imekuwa mstari katika kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi, hivyo ni wajibu wa watendaji na viongozi waliopo kuhamasisha, kusimamia na kufuatilia miradi hiyo kwani inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ina imani na matarajio makubwa kuona miradi yote ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inachangia ipasavyo juhudi za Serikali katika kuongeza uhakika wa chakula na kuleta maendeleo ya kijamii katika maeneo ya utekelezaji.
“Serikali ya Awamu ya sita inaendelea kutafuta fedha za kutekeleza miradi. Natoa rai kwa watendaji na viongozi wa halmashauri zote zinazotekeleza miradi ya mazingira kuhakikisha zinaimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi kuanzia ngazi ya Kata hadi vijiji,” amesema Dkt. Switbert.
Pia, ameweka wazi kuwa katika kuongeza juhudi za kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kisera na kimkakati ikiwemo Mkakati wa Kikanda (Afri 100) ambao unalenga kurejesha ekari Milioni 100 za misitu na ardhi zilizoharibika, ambapo kupitia Mkakati huo Tanzania imepanga kurejesha ekari Milioni 5.2 ifikapo mwaka 2030.
Ameongeza kuwa katika kufikia malengo hayo, Serikali imeanzisha miradi mbalimbali ya mazingira ikiwemo Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai Tanzania ulioanza mwaka 2021-2025 na kutekelezwa katika Halmashauri za Wilaya saba nchini zilizopo katika Mabonde ya Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa.
Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni Mpimbwe, Tanganyika, Sumbawanga, Mbeya, Mbarali, Wanging,ombe na Iringa na kuipongeza Halmashauri ya Mpimbwe kwa juhudi ilizofanya katika kutekeleza mradi huo ikiwemo kutenga ekari 732 kwa ajili ya uanzishaji wa msitu wa hifadhi ya mazingira unaojikita katika uanzishaji wa biashara ya kaboni.
Kwa upande wake Mratibu kitaifa wa mradi huo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Damas Mapunda amesema mradi huo ulioanza mwaka 2021- 2026 unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia GEF ukiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 11.2 umelenga kuimarisha usimamizi wa pamoja wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika ili kuleta ustawi wa mifumo-ikolojia.
Amesema ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais mbali na kukagua utekelezaji wa mradi pia amekabidhi vitendea kazi ikiwemo pikipiki saba kwa halmashauri zinazotekeleza mradi huo zenye thamani ya TZS Milioni 36.2 pamoja na mizinga ya 208 ya kuniria na kuchakata asali kwa vikundi vinne vya ufugaji nyuki vilivyopo Kata ya Kasasa.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, takribani hekta 110,000 za uoto wa asili zinatarajia kurejeshwa nchini ambapo kila halmashauri iliyotekeleza mradi huo imepangiwa eneo lake la utekelezaji kulingana na ukubwa wa jiografia, ambapo hadi sasa Halmashauri ya Mpimbwe imeotesha miche 230,000 ya miti pamoja na kuanzisha mashamba katika shule za msingi.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha IWUKI Wanawake, kilichopo kijiji cha Kikonko Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi Bi. Siwema Malima, ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwapatia vitendea kazi hivyo ikiwemo mizinga ya nyuki ambayo itawasaidia kurinia asali na kuchakata mazao ya nyuki kwa ufanisi na hivyo kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha jamii kuhusiana na kulinda na kuhifadhi mazingira.