………………….
Na. Sixmund Begashe
Program ya Sanaa na Wasanii (Museum Art Explosion (MAE) inayoendeshwa na Makumbusho ya Taifa kupitia Kituo chake Cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam, imeendelea kuwa gumzo kwa wadau wa sanaa na utamaduni nchini pamoja na watalii wa ndani na wa kimataifa, kutokana na kuwa zao la utalii wa kiutamaduni lililojaa ubunifu waki la aina.
Akiizungumzia program hiyo ya MAE, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini (TAFCA) Bw. Adrian Nyangamale licha ya kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuindesha program hiyo, amesema wao kama wadau wa sanaa na utamaduni wataendelea kushiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo kwa kuwa yana mchango mkubwa kwa wasanii na nchi kwa ujumla.
“Program hii inaendana na kasi ya Filamu ya The Royal Tour ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alishiriki kama muhusika Mkuu, Sasa tunaona watalii wengi wanakuja nchini hivyo wanapokuwa hapa Jijini Dar es Salaam wanapata fursa ya kuufurahia utamaduni wetu kupitia maonesho ya MAE” Aliongeza Bw. Nyangamale.
Naye Bi Neema Faraja, akiwa na watoto wake kwenye maonesho hayo yanayofanyika kila Ijumaa ya Mwisho wa mwezi, amesema yanawapa nafasi watoto kujifunza na kuurithi utamaduni wa Mtanzania, na kutoa wito kwa wazazi wengine hasa wa Mkoa wa Dar es Salaam kutumia maonesho hayo kuwarithisha watoto wao utamaduni wa kitanzania kwa kuwa ni rafiki kwa rika zote
Maonesho ya Mwezi wa Machi 2023 yalipambwa na Wasanii wa Mtandao wa Wasanii Wanawake Tanzania pamoja na Wasanii wa Muziki wa asili yenye maadhi ya Mkoa wa Mbeya cha “Wamwiduka” pamoja na vyakula mbalimbali.