Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Khadija Ali akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga, wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo iliyolenga kukagua miradi ya TASAF wilayani humo.
Katibu wa Kikundi cha Umoja ni Nguvu, Bi. Halima Mtulia akitoa taarifa ya maendeleo ya kikundi chao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo katika Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga, iliyolenga kukagua utekelezaji miradi ya TASAF.
……………………..
Na. James K. Mwanamyoto-
MkurangaTarehe 01 Aprili, 2023 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka waratibu wa TASAF wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanawapatia taarifa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhusu kiasi cha fedha kinachopokelewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya TASAF, ili kuwawezesha viongozi hao kusimamia vema na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo katika maeneo yao ya Utawala.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo akiwa wilayani Mkuranga, wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kiparang’anda alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.
Mhe. Jenista amesema, imekuwa ikitokea mara nyingi fedha za kutekeleza miradi ya TASAF zinawasilishwa katika Mikoa na Wilaya lakini Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanakuwa hawana taarifa rasmi, hivyo ni jukumu la waratibu wa TASAF katika ngazi za Mikoa na Wilaya kuwajulisha viongozi hao.
“Naendelea kuelekeza kila fedha ya TASAF inapopokelewa mkoani au wilayani, ni lazima Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wapewe taarifa zinazoanisha kiasi cha fedha kilichopokelewa ili iwe rahisi kwa viongozi hao kutekeleza jukumu la kuisimamia na kuifuatilia miradi yote ya TASAF,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, miradi yote ya TASAF inatakiwa kukamilika kwa wakati kama ambavyo miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inavyokamilika kwa wakati.
Aidha, Mhe. Jenista amevipongeza vikundi vya Walengwa wa TASAF wilayani Mkuranga baada ya kujionea bidhaa mbalimbali wanazozizalisha kwa kujishughulisha na ujasiriamali kwa lengo la kujiongezea kipato kitakachoboresha maisha yao.
Sanjari na hilo, Mhe. Jenista ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Mkuranga kwa kuamua kusimamia uanzishaji wa vikundi vya TASAF katika kila kata ili wananchi wanufaike na fedha za TASAF ikiwa ni pamoja na mikopo ya Halmashauri inayotolewa kwa wanachi walio katika vikundi.
“Sote ni mashaidi hapa, tumeona vikundi hivi vya walengwa wa TASAF namna vilivyozalisha mikeka, unga wa muhugo, batiki na fagio hivyo vimekuwa ni mfano bora wa kuigwa na wananchi na vikundi vingine nchini,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Khadija Ali amesema akina mama waliounda vikundi vya TASAF katika wilaya yake wamekuwa mstali wa mbele katika kuhakikisha watumia vema ruzuku wanayoipata kuendesha miradi waliyoibuni kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Mhe. Khadija amesema, miradi mingi ambayo akina mama wilayani kwake wameiibua itaendelea kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa ndani ya wilaya ya Mkuranga, akitoa mfano wa uzalishaji wa unga wa muhogo, fagio na mikeka ambao unaendana na dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini.
Naye, Katibu wa Kikundi cha Umoja ni Nguvu, Bi. Halima Mtulia amesema TASAF imewawesha kupata mafunzo ya kutengeneza fagio za chelewa ambayo yameongeza thamani ya zao la minazi na kuongeza kuwa, kikundi chao kimepata eneo la kufanyia shughuli za biashara pamoja na kumpata mfadhili wa kujenga eneo maalum la kufanyia biashara.
Mhe. Jenista Mhagama amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja Wilayani Mkuranga, iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini ambao unaratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).