Afisa Mkuu wateja wakubwa na serikali ,Alfred Shao akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo jijini Arusha leo
Kamishna wa TFS kanda ya kaskazini SACC ,Edward Shilogile akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo jijini Arusha leo.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru,Emmanuela Kaganda akipanda mti katika chuo cha ufundi Veta Oljoro katika uzinduzi wa mradi huo jijini Arusha leo
……………………………
Na Julieth Laizer
Arusha.Benki ya NMB kwa kushirikiana na Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) imezindua rasmi kampeni ya upandaji miti katika taasisi mbalimbali na shule kwa lengo la kuotesha miche milioni 1 kwa nchi nzima kwa mwaka 2023.
Aidha uzinduzi wa mradi wa upandaji miti kwa kanda ya kaskazini umezinduliwa katika Chuo cha ufundi Veta Oljoro kwa kupanda miche ya miti 5,000 wakati benki hiyo ikitimiza miaka 25 .
Akizungumza wakati wa kuzindua kampeni hiyo chuoni hapo ,Afisa Mkuu wateja wakubwa na serikali wa benki hiyo,Alfred Shao amesema kuwa benki hiyo wamefikia hatua ya kufanya hivyo ikiwa ni sehemu mojawapo ya kurudisha faida wanayoipata kwa jamii kwa kupanda miche ya miti hiyo kwa lengo la kuhifadhi na kutunza mazingira.
Amesema kuwa,zoezi hilo la upandaji na utunzaji miti kwa kanda ya kaskazini ni endelevu baada ya kuzinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Philip Mpango lililozinduliwa kitaifa jijini Dodoma.
Shao amesema kuwa, benki hiyo mwisho mwa mwezi wa januari mwaka huu walitangaza faida ya kihistoria ambayo benki ya NMB ilipata kwa mwaka 2022 ambapo kutokana na faida hiyo Benki walitangaza rasmi kutenga shs bilioni 6.2 kwa ajili ya kurejesha kwa jamii .
Amesema kuwa , kwa upande wa kanda ya kaskazini katika programu hiyo ya kupanda na kutunza miti watapanda miti 250,000 kwa mikoa ya Arusha,Kilimanjaro ,Manyara na Tanga kwa mwaka huu 2023.
Aidha amefafanua kuwa ,ili kufanya miti watakayoipanda ikue na kuleta matokeo changa,wameandaa shindano la upandaji miti mashuleni litakalotambulika kama “Kuza mti Tukutunze” kwa shule mbalimbali za Tanzania bara na visiwani ambapo zitashindana kupanda na kutunza miti watakayokabithiwa ndani ya mwaka mmoja na nusu.
“Katika mashindano hayo shule itakayokuwa mshindi wa kwanza katika upandaji na utunzaji miti itazawadiwa shs milioni 50,hii ni shule ambayo itakuwa imepanda miti 2,000 na kufanikiwa kukuza asilimia 80 na zaidi ya miti yote waliyopanda,huku mshindi wa pili akizawadiwa shs milioni 30 kwa shule ambayo itaweza kupanda miti 1,500 na kukuza kwa asilimia 70 na zaidi ya miti yote waliyopanda.”amesema .
Aidha kwa upande wa mshindi wa tatu atazawadiwa shs milioni 20 huku akitakiwa kupanda miti 1,000 na kufanikiwa kukuza asilimia 70 na zaidi ya miti yote waliyopanda.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha amesema kuwa,ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha napanda na kuhifadhi miti kwa ustawi wa Taifa kwani inasaidia kupunguza mmomonyoko wa ardhi na kusaidia kuhifadhi mazingira na kujikinga na upepo mkali.
Aidha ameyataka makampuni binafsi na taasisi kuwa mfano bora wa kuigwa kwa upandaji miti kwa kuonyesha kwa vitendo sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali katika upandaji miti.
Naye Kamishna wa TFS kanda ya kaskazini,SACC Edward Shilogile amesema kuwa, lengo la mpango huo ni kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwa zoezi hilo ni endelevu na wataendelea kutoa miche ya kutosha kwa ajili ya taasisi mbalimbali na kwenye mashule pia