Machi 31, 2023
Na Zillipa Joseph, Katavi
Jamii imehamasika kuandikisha watoto wenye mahitaji maalum kujiunga na elimu ya darasa la awali na darasa la kwanza katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kufuatia uhamasishaji unaoendelea kufanywa katika jamii juu ya kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum.
Hayo yamesemwa na Mwalimu Mkuu Msimamizi wa Kitengo cha Elimu Maalum katika shule ya msingi Azimio bwana Frank Kasagula ambapo amesema kuwa hata kitendo cha serikali kuwapatia chakula cha mchana watoto hao wawapo shuleni kimesaidia watoto hao wenye mahitaji maalum kuhudhuria kila siku na kupenda shule.
Aidha mwalimu Kasagula ametaja uwepo wa miundombinu rafiki ya vyoo katika shule hiyo, pamoja na uwepo wa vifaa vya kutosha vya kujifunzia na kufundishia sanjari na vifaa vya upimaji; vilivyotolewa na serikali na mashirika binafsi yanayotekeleza mpango wa Elimu Jumuishi.
Ameongeza kuwa kupungua kwa mitazamo hasi ya wanajamii juu ya watu wenye mahitaji maalum imepelekea kuongezeka kwa wanafunzi wanaoandikishwa katika shule hiyo kwani wazazi na walezi wamekuwa wakipeleka watoto wao kupata vipimo katika shule hiyo, na kuwaandikisha kuanza masomo.
Mafanikio mengine aliyotaja mwalimu Kasagula ni pamoja na kuongezeka kwa ufaulu wa watoto hao katika mitihani yao akitaja kuwa hili linatokana na watoto hao kutonyanyapaliwa na jamii na hivyo kushiriki vyema katika masomo yao.
Akielezea changamoto zilizopo mwl. Kasagula amesema kukosekana kwa bweni katika kitengo hicho kunawakosesha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaoishi mbali na kituo kutokupata fursa ya kupata elimu, pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa ambapo vyumba vilivyopo ni vitatu huku kukiwa na wanafunzi wa darasa la awali mpaka darasa la saba, hali inayopelekea wanafunzi wa madarasa tofauti kuchanganywa katika darasa moja.
Aidha chumba cha upimaji hakina ubora licha ya kuwa ndio kituo cha upimaji cha mkoa kwani ni jengo chakavu, huku akitaja mtaala unaotumika kufundishia watoto hao kuwa sio rafiki na kuziomba mamlaka zinazohusika kubadilisha mtaala wa masomo ili wapate mtaaala rafiki kwa watoto wenye ulemavu.
Kitengo hicho cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Azimio kilianzishwa mwaka 2003 kinahudumia jumla ya watoto jumla ya watoto 39 kati yao wakiwemo wanafunzi wanne wasioona ambapo kituo kinahudumia watoto viziwi na wasioona.
Kwa mwaka 2023 watoto wenye mahitaji maalum wa darasa la awali walioandikishwa ni sita wakiwemo wavulana wawili na wasichana wanne; huku na darasa la kwanza wameandikishwa wavulana wawili na wasichana watatu jumla watano tofauti na miaka ya nyuma ambapo kuwapata watoto hao ili kujiunga na shule ilikuwa ni mpaka kuwatafuta mahali wanapoishi.
Kwa sasa shule hiyo inaendelea na ujenzi wa bweni ambapo wamepokea kiasi cha shilingi milioni 25 kutoka serikalini, lakini kwa mujibu wa mwalimu Kasagula fedha hizo hazitatosha kukamilisha ujenzi wa bweni hilo hivyo amewaomba wadau kuchangia ujenzi huo ili watoto wenye mahitaji maalum wanaoishi maeneo ya mbali wapate fursa ya kupata elimu.
Fortunata Kabeja mwenyekiti UWT kutoka Chama cha Mapinduzi kwa mkoa wa Katavi, amesema watoto wenye mahitaji maalum ni sehemu ya jamii ambapo wanapaswa kupendwa na kutotengwa ili wajisikie vizuri kama wanajamii wengine.
Ameitaka kamati ya shule kushirikisha jamii katika kuchangia ujenzi wa vyumba vingine vya madarasa ili kupunguza changamoto iliyopo pamoja na bweni kwani fedha zinazotolewa na serikali katika ujenzi wa bweni linaloendelea kujengwa shuleni hapo bado hazitoshelezi.
Bi. Anna Sawasawa ni afisa Elimu, Elimu Maalum Manispaa ya Mpanda, amesema kituo cha upimaji cha Azimio kinapima macho, masikio na ulemavu wa akili na kuwaomba wadau kuchangia kukiboresha chumba cha upimaji kiwe na hadhi kwani vifaa vya upimaji vipo.
Ameongeza kuwa manispaa ya Mpanda itajitahidi kwa uwezo wake kuongeza walimu katika kituo hicho ambacho kwa sasa kina walimu 6 kitengo cha viziwi; huku walimu wa wasiiona wakiwepo wawili ili kuwapunguzia mrundikano wa vipindi.
Baadhi ya wazazi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi wamesema wamehamasika kuwapeleka watoto shule kwani inasaidia kuwachangamsha watoto wao.
Bi. Pili Mfaume mkazi wa Mpanda mjini, amesema anaona mabadiliko chanya kwa mjukuu wake anayesoma katika shule hiyo, na kuongeza kuwa muda mtoto akiwa shuleni kunampatia uhuru wa kufanya kazi zake.
Kwa upande wao watoto hao walionekana kufJAMII IMEHAMASIKA KUANDIKISHA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMurahia wageni ambapo mtoto mmoja alijitolea kuimba wimbo wa kuwasifu wageni waliofika shuleni hapo kuwatembelea akisema wamependeza na wanavutia na kuwakaribisha tena kufika shuleni hapo kuwaona.