Mkuu wa wilaya ya Arusha,Felician Mtahengerwa akizungumza na wafanyakazi hao baada ya kufanya mgomo kwa siku mbili jijini Arusha .
Mwenyekiti wa makampuni ya Lodhia ,Arun Lodhia akizungumza na wafanyakazi hao jijini Arusha leo
Mwenyekiti wa makampuni ya Lodhia ,Arun Lodhia akizungumza na wafanyakazi hao jijini Arusha leo
……………………………………….
Julieth Laizer, Arusha.
Arusha.HATIMAYE mgomo uliokuwepo kati ya wafanyakazi wa kampuni ya kuchakata chuma na kuzalisha nondo cha Lodhia na uongozi umemalizika baada ya uongozi wa wilaya kuingilia kati swala hilo na hivyo wafanyakazi hao kushughulikiwa changamoto zao .
Aidha wafanyakazi hao walikuwa wakilalamikia kulipwa kiwango kidogo cha mshahara huku ikilinganishwa na kazi ngumu wanayofanya katika kampuni hiyo.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Arusha ,Felician Mtahengerwa wamesema kuwa wamekuwa wakiahidiwa kuongezewa mishahara kila mwezi lakini makubaliano hayo yamekuwa hayafanyiwi kazi.
Mmoja wa wafanyakazi hao ,Martin Antony amesema kuwa ni muda mrefu sasa tangu waombe kuongezewa mshahara kwani kwa mwezi wanapokea shs 150,000, kiasi ambacho hakitoshelezi kwa mahitaji yao ya kila siku.
Aidha wafanyakazi hao wamelalamikia pia kitendo cha kutokulipwa overtime kwa muda mrefu kitendo ambacho kinawakatisha tamaa katika utendaji wao wa kazi.
Pamoja na hayo hawakusita kulalamikia vifaa duni vya utendaji kazi wakati wa ufanyaji kazi kwani wengi wao wamekuwa wakilazimika kwenda soko la Samunge kujinunulia viatu vya kuwakinga na majanga katika maeneo ya kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa makampuni ya Lodhia ,Arun Lodhia amesema kuwa , amesikiliza changamoto zote na wamekaa na uongozi na kukubaliana mshahara utakuwa 180,000 badala ya 150,000 iliyokuwepo awali na watalipwa pamoja na overtime hapo hapo.
“Na changamoto zingine zote ndogondogo zinafanyiwa kazi nawaombeni sana mjitahidi kufanya kazi kwa bidii nitawapandisha cheo maana kampuni ni yetu sote tupambane kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa kwa maendeleo ya kiwanda na sisi kwa ujumla.”amesema.
Aidha amesema kuwa,watakuwa wanakutana kwa mwaka mara mbili ili kuweza kusikiliza kero na changamoto mbalimbali za wafanyakazi na kuweza kuzifanyia kazi ili kuondokana na migogoro mbalimbali isijitokeze tena.
Naye mkuu wa wilaya ha Arusha ,Felician Mtahengerwa amesema kuwa,anashukuru uongozi huo kumaliza mgogoro huo na kuweza kuwaongezea mshahara kama walivyotaka jambo ambalo linaleta ufanisi mkubwa mahala pa kazi.
Aidha amewataka wafanyakazi hao kuacha wizi badala yake waheshimu sehemu yoyote ambayo inawapatia inawapatia riziki.
“Mimi mwenyewe nitakuja kufuatilia yale yote tuliyokubaliana kuhakikisha haki inatendeka leo nendeni mkapumzike kesho muingie kazini rasmi na ongezeni bidii katika utendaji kazi wenu ili muwe mfano bora wa kuigwa.”amesema