Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2021/2022 kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Charles Kichere, Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 29 Machi, 2023.
………………………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
amewaagiza viongozi na watendaji wa Serikali kuzisoma na kuzielewa vyema taarifa
za rushwa na za ukaguzi wa hesabu za Serikali ili ziwasaidie kujitathmini.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo mara baada ya kupokea taarifa ya Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) katika hafla iliyofanyika Ikulu.
Aidha, Rais Samia amesema taarifa hizo hizo zinasaidia kusimamia na kuimarisha
utawala bora na kuhakikisha udhibiti na usimamizi wa rasilimali za Serikali
unafanywa kikamilifu.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Bandari kufanya kazi na
sekta binafsi ili kuimarisha mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji fedha ambapo
itasaidia kudhibiti upotevu mkubwa wa fedha unaotokea bandarini.
Rais Samia pia amegiza kufanyiwa tathmini kwa Mashirika ya Umma yaliyopata
hasara na kuyafuta Mashirika ambayo hayana tija kwa taifa kwa kuwa Mashirika
hayo yanatumia gharama kubwa lakini hayaleti faida kwa Serikali.
Katika ripoti ya CAG jumla ya Halmashauri 14 nchini zimepata hati zenye mashaka
zikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Babati, Bahi, Geita, Kilindi, Mbinga,
Musoma, Nkasi, Nyasa, Simanjiro, Songwe, Sumbawanga Manispaa pamoja na
Ushetu.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2021/2022 kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo CP. Salum Hamduni Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 29 Machi, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali mara baada ya kupokea Taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taarifa ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2021/2022, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Machi, 2023.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya kupokea Taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taarifa ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2021/2022, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Machi, 2023.