WANANCHI wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameiomba serikali kupitia wizara ya afya kuwa na utaratibu wa kutembelea mara kwa mara maeneo ya vijijini kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzina upimaji wa vimelea vya ugonjwa kifua kikuu na kuwaanzishia dawa watakaobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Wametoa ombi hilo jana,wakati wa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa huo iliyofanywa na wataalam kutoka Hospitali ya wilaya Tunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo shirika lisilo la Kiserikali la MDH-Amref Health Africa.
Kampeni imefanyika katika kijiji cha Chingulungulu kata ya Muhuwesi na kuhudhuriwa na wananchi kutoka vijiji vya kata jirani ya Majimaji,Sisi kwa Sisi iliyoambatana na maadhimisho ya siku ya kifua kikuu Duniani ambayo kimkoa imefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ngatuni wilayani Tunduru.
Hadija Jaribuni alisema,utaratibu wa kupeleka huduma za uchunguzi wa afya kwa wananchi waishio maeneo ya pembezoni ni nzuri sana kwani utasaidia kuokoa maisha ya watu wengi hasa wanaoishi maeneo hayo ambayo ni nadra sana kufikiwa na huduma hizo kwa wakati.
“naishukuru sana serikali kupitia Hospitali ya wilaya Tunduru kitengo cha kifua kikuu na ukoma kutuletea huduma ya uchunguzi,tunaomba wataalam wafike mara kwa mara”alisema Jaribuni.
Ameishukuru serikali kupeleka
huduma hiyo kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kwenda Hospitali na vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya zao na kupata matibabu.
Shamila Said alisema,kufikishwa kwa huduma ya uchunguzi kwenye maeneo ya vijijini itasaidia sana kuokoa maisha ya watu wengi hasa wazee ambao hawawezi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa nauli ya kutoka kijijini hadi Hospitali ya wilaya Tunduru mjini.
Alisema,huduma ya uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu ni nzuri kwani inatoa majibu ya shida za wananchi wenye maradhi ambao wana tabia ya kumeza dawa bila kupata ushauri wa Madaktari.
Diwani wa kata ya Muhuwesi Iman Ngonyani alisema,wananchi wa kijiji cha Chingulungulu wameanza ujenzi wa zahanati ambayo mara itakapokamilika itasaidia kutoa huduma mbalimbali za matibabu ikiwemo huduma ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu.
Ngonyani,amewapongeza watoa huduma kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwataka kuendelea kuwasaidia wananchi ambao bado wanakabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha na maradhi ya mara kwa mara.
Kwa upande wake Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,katika kampeni ya mwaka huu nguvu kubwa imeelekezwa kutoa elimu ya kifua kikuu kwa wanafunzi kutokana na kundi hilo kuwa katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo.
Alisema,wanafunzi wakipata elimu kuhusu ugonjwa huo itakuwa rahisi kuchukua tahadhari na hata kupeleka elimu hiyo kwa wazazi wao na jamii kwa ujumla.
Dkt Mkasange aliyataja makundi mengine yaliyoko kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa TB ni wafugaji,wasafiri,wafungwa,watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na wale wanaishi kwenye makazi duni.
Mkasange,ameitaka jamii kuwa na utaratibu wa kwenda katika vituo vya kutolea huduma na Hospitali kwa ajili ya uchunguzi ili kufahamu hali za afya zao badala ya kuwa na mazoea ya kumeza dawa bila kupata ushauri wa wataalam
MWISHO.